Keifo FM

Kyela:Mtendaji ayatapika mamilioni ya Kafundo mbele ya Katule.

26 May 2025, 13:14

Pichani ni mwenyekiti wa halmashauri ya Kyela Katule Kingamkono akiwa kwenye kikao cha mrejesho kurudisha fedha za wananchi picha na James Mwakyembe

Zaidi ya shilingi milioni tano zilizofujwa na mtendaji wa kijiji hicho zimerejeshwa kwenye akaunti ya kijiji hicho na kuelekezwa kwenye miradi mipya ya kijiji cha Kafundo.

Na James Mwakyembe

Hatimae mwenyekiti wa halmashauri ya Kyela Katule Kingamkono kwa kushirikiana na timu ya watalaam wamefanikisha kuzirejesha fedha za miradi ya kijiji cha kafundo zaidi ya shilingi milioni tano zinazodaiwa kutumika vibaya na mtendaji wa kijiji hicho mapema mwaka huu.
Ubadhirifu huo uliibuliwa na wananchi wa kijiji hicho mwanzoni mwa mwaka huu katika ziara ya kikazi ya Mwenyekiti wa halmashauri ya Kyela akiwa na timu ya wataalam hali iliyomlazimu kuagiza mkaguzi wa hesabu za serikali kukagua ili kujiridhisha na malalamiko hayo hali iliyopelekea kubainika upotevu wa kiasi cha zaidi ya shilingi milioni tano za kitanzania.
Akizungumza leo wakati wa mkutano wa mrejesho wa malalamiko hayo Katule amesema lengo la serikali ni kuhakikisha suala la utawala bora linakuwa sehemu ya utamaduni uliozoeleka hapa wilayani kyela huku akisisitiza kuwa hakuna kiongozi wa serikali atakayevumiliwa baada ya kubainika katika matumizi mabaya ya fedha za wananchi.

Sauti ya Katule kuhusu fedha kurudi 11

Baada ya kuzirejesha fedha hizo za wananchi na kuziingiza katika akaunti ya kijiji cha kafundo Katule ametoa maelekezo kwa viongozi wa Kijiji na Kata hiyo kuhakikisha wanazipangia matumizi fedha hizo ili ziweze kutumika katika miradi ya maendeleo kijijini hapo pamoja na kuwatoa hofu juu ya mtendaji huyo kuwa hatakuwa sehemu ya wapanga mipango ya matumizi ya fedha hizo.

Sauti Katule kuhusu matumizi ya fedha 22

Kwa upande wa wananchi wa kafundo wao wamemshukuru mwenyekiti wa Halmashauri ya Kyela kwa jitihada zake za kuhakikisha fedha zao zinarudi na kuwaomba viongozi kuzielekeza katika matumizi ya kununua vifaa katika shule ya Msingi kafundo ili kuwaondolea mzigo wazazi wakati wa mitihani.

Sauti ya wananchi kafundo kuhusu Shukrani 33
Pichani wananchi wa kijiji cha Kafundo wakiwa kwenye mkutano wa hadhara kusubiri mrejesho wa fedha zao

Kijiji cha Kafundo ni moja ya vijiji vinavyounda kata ya Ipinda na ni kijiji chenye historia kubwa inayojengwa na uwepo wa mashamba makubwa ya kijiji tangu ujamaa jambo ambalo limeifanya Kafundo kuwa tajiri wa miradi ya kimaendeleo.