Kyela: Manase mgeni rasmi kilele cha Sheria Kyela
31 January 2024, 22:29
Mkuu wa wilaya ya Kyela Josephine Manase anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika maadhimisho ya siku ya sheria hapo kesho katika viwanja vya mahakama ya wilaya ya Kyela.
Na Nsangatii Mwakipesile
Kuelekea kelele cha maadhimisho ya siku ya sheria hapa nchini hakimu mkazi mfawidhi mahakama ya wilaya ya Kyela Severin Njau amewaomba wananchi kujitokeza kwa wingi katika maadhimisho hayo yatakayofanyika katika viwanja vya mahakama ya wilaya Kyela.
Hakimu huyo mfawidhi Severin Njau amesema katika maadhimisho hayo mgeni rasmi ni mkuu wa wilaya ya Kyela Josephine Manase akiwa na jopo zima kutoka halmashauri ya wilaya ya Kyela.
Pia amebainisha kuwa kabla ya maadhimisho hayo kufikia kilele hapo kesho tayari watalaamu kutoka mahakama mbalimbali hapa wilayani Kyela walioambatana na wadau wengine wa masuala yahusuyo sheria wamezunguka katika shule takribani tano kutoa elimu ya sheria kwa wanafunzi na walimu ambapo zaidi ya wanafunzi elfu mbili wamenufaika na elimu hiyoKye.
Ametumia muda huo kuwashukuru wadau hao waliojitokeza kwa kufanikisha mpango huo ambao ameutaja kuwa na mafanikio kuelekea hapo kesho ambapo itakuwa ndiyo kilele cha wiki ya sheria iliyoanza tarehe 24 januari 2024 na kufikia kikomo hapo kesho 1 februari 2024.
Maadhimisho ya sheria huadhimishwa kila mwaka kuanzia tarehe 24 januari hadi 1 februari kila Mwaka ikiashiria kufunguliwa kwa msimu mpya wa mahakama hapa nchini Tanzania.