Kyela waunda Chamata
8 January 2024, 15:47
Wakati Raisi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan akiendelea na jukumu la kuwaletea maendeleo wananchi wa Tanzania, wadau mbalimbali wa maendeleo hapa wilayani Kyela wameunda umoja wao unaotambulika kwa jina la Chamata Tanzania ukiwa na lengo la kupaza sauti ya Samia Suluhu Hassan kwa watanzania.
Na Nsangatii Mwakipesile
Kikao cha kwanza cha taasisi ya Chamata wilaya ya Kyela kimefanyika huku wajumbe na washiriki wa kikao hicho wakipongeza na kuutaka uongozi huo mpya kuhakikisha unasimamia ajenda kuu ya kumsemea Samia Suluhu Hasani Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa watanzania wapenda maendeleo.
Haya yanajiri ikiwa ni siku chache tu tangu uongozi wa wilaya ya Kyela kuchaguliwa na kuwekwa madarakani kwa mujibu wa katiba ya Chamata ambapo baada ya kuchaguliwa viongozi hao wameanza moja kwa moja kutekeleza majukumu yao kama wanavyotakiwa.
Akizungumza mara baada ya kukamilika kwa kikao kazi cha taasisi hiyo katibu mkuu wa Chamata wilaya ya Kyela Imani Mwambusye amesema lengo la kikao hicho ilikuwa ni utambulisho wa viongozi pamoja na kuitambulisha Chamata kwa wajumbe ili kila mtu ajue namna iliyo bora ya kumsemea Mama Samia Suluhu Hassan.
Kwa upande wao washiriki wa kikao hicho ambao pia ni wajumbe na wananchama wa Chamata wamesema kitendo cha taasisi hiyo kufika kyela kwao ni jambo ambalo lilichelewa hivyo kuahidi kwa wapo tayari kuhakikisha wanakuwa sauti ya Mama kila walipo na waendako.
Wakizungumzia kuhusu utendaji kazi wa Rais Samia wajumbe hao wamesema hakuna shaka katika hilo kwani wilaya ya kyela ni miongoni mwa wilaya zilizopewa kipaumbele na serikalai ya awamu ya sita hasa kwa kuzingatia kuwa miradi mikubwa bandari kavu ya Kasumulu,ujenzi wa barabara ya Ibanda Itungi-Kiwira na mingine mingi imeendelea kutekelezwa kwa kasi kubwa ndani ya wilaya ya Kyela.
Taasisi ya chamata ni taasisi mpya iliyosajiriwa kisheria ambayo majukumu yake makubwa ni kuhakikisha wanakuwa sauti ya Mama Samia Suluhu Hasani Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kazi kubwa ya anayoifanya ya kutekeleza miradi mikubwa ya kimkakati na ile ya kawaida kuhakikisha watanzania wote wanazitambua kazi hizo zilizotukuka kutokana na kuwepo baadhi ya wanasiasa wachache kupotosha wananchi juu ya ukweli huo.