Kyela:Serikali kumtua ndoo mwanamke Kyela
27 December 2023, 20:03
Jumla ya shilingi bilioni nne zimetolewa na serikali ya Tanzania kwa wananchi wilayani Kyela ili kukamilisha mradi wa ujenzi wa mtandao wa maji safi na salama kutoka halmashauri ya Busokelo.
Na Masoud Maulid
Wananchi wilayani Kyela wameanza kuwa na matumaini ya kupata maji safi na salama kutoka chanzo cha maji Mbambo hadi Kyela mjini baada ya ahadi za muda mrefu.
Wakizungumza na mwandishi wa habari wananchi wa kata ya Ipande,Nkonkwa,Mwaya na Kyela mjini wamesema kutokana na jitihada zinazoendelea, za utandazaji wa mabomba kutoka chanzo cha maji Mbambo halmashauri ya Busokelo hadi kufika kata ya Mwaya kijiji cha Malungo,ni hatua ambayo imeleta matumaini kwa wananchi kuondokana na kilio cha maji.
Kwa upande wake Kenethi Kalolo Mpingo mkazi wa kijiji cha Kapamisya amesema mpaka sasa hatua iliyofikia inaridhisha kwa kuwa ahadi za viongozi waliotangulia zilikuwa nyingi japo utekelezaji wake haukuonekana hasa kwenye swala la maji hivyo wameipongeza serikali ya Mama Samia na kumshukuru Mbunge wa jimbo la Kyela kwa kulipigania hadi kufikia hatua iliyopo kwa sasa
Nae Bupe Kabona mkazi wa kijiji cha Malungo wilaya ya Kyela amesema mbunge wa jimbo la Kyela Ally Mlaghila Jumbe Kinanasi katika kipindi cha kampeni za uchaguzi wa mwaka 2020 aliahidi kushughulikia changamoto ya upatikanaji wa maji kwa wilaya Kyela ambapo jitihada zake zinakwenda kuondoa adha ya wa wanawake kutembea umbali mrefu kuyafuata maji.
Mradi wa maji kutoka Mbambo hadi Kyela mjini utakaoghalimu kiasi cha zaidi ya shilingi bilioni nne utawanufaisha zaidi ya wananchi laki tatu wanaoishi ndani ya Mamlaka ya mji mdogo wa Kyela kwa kupata maji safi na salama.