Kyela:Kinanasi kutunukiwa Uchifu wilaya ya Kyela
18 December 2023, 12:54
Mbunge wa jimbo la Kyela Ally Mlaghila Jumbe Kinanasi anatarajiwa kuvikwa uchifu na jumuaiya ya wazee wa kimila wilaya ya kyela katika tukio litakalofanyika desemba 28 mwaka huu.
Na Masoud Maulid
Umoja wa wazee wa kimila maarufu Machifu na wasaidizi wao maarufu mafumu wilaya ya kyela wamekusudia kumtunuku mbunge wa jimbo la kyela Ally Mlaghila Jumbe Kinanasi cheo cha kuwa mlezi wa Machifu wilayani hapa.
Akizungungumza na mwandishi wa habari mwenyekiti wa machifu wilaya ya kyela Uswege Grant Mwakabulufu amesema kusudi la machifu kumtunuku mbunge kuwa mlezi wa machifu linatokana na jitihada zake za kuwapenda wazee na kupenda kuendeleza utamaduni.
Chifu Mwakabulufu ameongeza kuwa kutokana na sherehe hiyo itakayofanyika disemba 28 mwaka huu katika kijiji cha kikuba kata ya lusungo kuwa wanatarajia kufanya sherehe kubwa ambayo itashirikisha baadhi ya machifu kutoka nje ya kyela wakiwemo machifu kutoka mkoani Morogoro na nchi jirani ya Malawi.
Katika hatua nyingine chifu Mwakabulufu amebainisha kuwa sherehe hiyo itaambatana na burudani mbalimbali za ngoma za asili pamoja na shindano la kumpata kijana mnyakyusa atakayekuwa mahiri wa kutupa mkuki umbari mrefu.
Nae katibu wa machifu wilaya ya kyela Exavery Kamoma Mwamloba kutoka himaya ya chifu Koroso amesema kwa tukio hili mbunge amebarikiwa na mungu kwa kuwa ni tukio la kwanza kufanyika wilaya ya kyela ambapo wazo hilo lilianza mwaka 2022 na kumwandikia barua ya kumuomba kusimikwa kuwa mlezi wa machifu kwa wilaya ya kyela.
Kwa uapnde wake Samweli Mwalukuta akizungumza kwa niaba ya wasaidizi marufu mafumu amesema wanayo furaha kubwa kuandaa sherehe hizo kwa ajili ya kumvika kiongozi wa jimbo la kyela kuwa mlezi wao na kuwaomba wananchi wote kufika kwa wingi kushuhudia kitakachofanyika.
Wilaya ya kyela wazee wa kimila maarufu Machifu wanapatikana katika himaya nne,himaya ya Chief Mwakalukwa Chifu Mwakyembe,Chifu Mwakabulufu na Chifu Koroso ambapo wanadaidizi wao wanatambulika maarufu kwa jina la Mafumu.