Matukio ya udhalilishaji yaongezeka kwa 32.3% Zanzibar
23 August 2023, 2:53 pm
Na Ahmed
Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imesema pamoja na kupiga vita dhidi ya matukio ya udhalilishaji na ukatili kwa wanawake na watoto lakini bado matukio hayo yanaongezeka kila siku.
Kwa mujibu wa takwimu za makosa ya ukatili na udhalilishaji wa kijinsia kutoka ofisi ya mtakwimu mkuu wa serikali Zanzibar amesema kwa mwezi wa Julai matukio hayo yameongezeka kwa asilimia 32.3 kutoka matukio 127 kwa mwezi Juni 2023 hadi matukio 168 mwezi Julai.
Akiwasilisha takwimu hizo Mtakwimu kutoka Diviseheni na Ajira naJinsia, ya Ofisi ya Mtakwimu Mkuu Zanzibar Ramla Hassan Pandu amesema wilaya ya Magharibi “A” ndio kinara wa makosa hayo ambapo imeripotiwa jumla ya matukio 46 hiyo ikiwa ni sawa na asilimia 47.4 ya matukio yote ikifuatiwa na wilaya ya Mjini ambayo imeripotiwa matukio 40 sawa na asilimia 23.8 ya matukio yote.
Amesema wilaya hiyo ya Magharibi “A” imeripotiwa kuwa na idadi kubwa ya matukio ya kubaka ikilinganishwa na wilaya nyingine ambapo imeripotiwa jumla ya matukio ya kubaka23 sawa na asilimia 29.1 ya matukio yote ya kubaka ambayo ni 79.
Kwa upande wake Mkaguzi wa Polisi kutoka makao makuu ya Polisi Zanzibar Makame Haji Haji amewasisitiza wazazi na walezi juu ya suala zima la kuwachunga watoto ili kuepukana na matukio hayo.
Akizungumzia suala la kutofautiana kwa adhabu ya makosa hayo wakili kutoka ofisi ya mkurugenzi wa mashtaka Zanzibar Huda Othman amesema hukumu hutolewa kulingana na uzito wa ushahidi uliowasilishwa mahakamami.