Miaka mitatu ya ZCRF imesaidia Watoto Kujieleza Zanzibar
19 December 2024, 4:44 pm
Na Mary Julius.
Uwepo wa Jukwaa la Haki za Watoto Zanzibar (ZCRF) umesaidia watoto kuwa na uhuru wa kujieleza,kujitambua na kupelekea kushiriki katika jukwaa la bajeti Zanzibar.
Akizungumza wakati wa wakiwakilisha ripoti ya mwaka ya Jukwaa la Haki za Watoto Zanzibar (ZCRF) hafla iliyofanyika katika ukumbi wa Skuli ya Tumekuja, Mwenyekiti Wa Jukwaa Hilo Mussa Kombo amesema Watoto wameweza kuhusishwa katika majadiliano ya bajeti na kupata fursa ya kutoa maoni kuhusu vipaumbele muhimu kwao, kama vile huduma za afya, elimu bora, na usalama wao.
Aidha Mwenyekiti Mussa amesema uwepo wa jukwaa hilo umesaidia kuwaanzishwa kwa mfumo wa uwajibikaji wa jamii unaazingatia ushirikishwaji wa watoto.
Kwa upande wake Mratibu wa Jukwaa la Haki za Watoto Zanzibar Sophia Leghela amesema Mradi umefanikiwa kuhakikisha sauti za watoto zinasikika na kuweza kushiriki katika vikao mbalimbali vya maamuzi pamoja na kuwakutanisha na viongozi wa serikali na kuwakilisha changamoto zao.
Aidha Sophia amewataka wazazi kuwaruhusu watoto kushiriki katika mabaraza ili kujenga viongozi wazuri wa badae.
Nao watoto wanaoshiriki katika Jukwaa la Haki za Watoto Zanzibar (ZCRF) wamewataka watoto kujitokeza katika mabaraza ili kujijengea uwezo wa kujisimamia na kushiriki katika mambo mbalimbali yanayo wahusu.
Jukwaa la haki za watoto Zanzibar ni mwavuli wa asasi za kiraia Zanzibar ambazo zimejikita kwenye ulinzi na utetezi wa haki za watoto, jukwaa limeweza kuwafikia watoto 1028 wakiwemo wasichana 672 na wavulana 356.