Balozi Hamad aahidi kutangaza fursa za kitalii, kuimarisha uhusiano
11 December 2024, 4:58 pm
Na Omary Hassan.
Balozi Hamad Khamis Hamad amesema ataitumia nafasi ya Ubalozi kutangaza fursa mbalimbali zinazopatikana nchini ikiwemo Utalii pamoja na kuimarisha uhusiano ili kukuza maslahi ya Tanzania.
Akizungumza na Maafisa, Wakaguzi na Askari wa Jeshi la Polisi wa Mikoa mitatu ya Unguja katka hafla ya kuwaaga iliyofanyika Chuo cha Polisi Zanzibar ambapo ametumia nafasi hiyo kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kumuanini na kumteua kuwa Balozi.
Aidha amewahimiza Askari wa Jeshi la Polisi kuacha matumizi mabaya ya mamlaka waliyonayo na badala yake wafanye kazi kwa kuzingatia haki za binadamu.
Kwa upande wake Mkuu wa Chuo cha Polisi Zanzibar, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi Sacp. Moses Neckemiah Fundi amesema Balozi Hamad atakumbukwa kwa kukemea rushwa, kuwasihi Askari kuheshimu haki za binaadamu na kufanya kazi kwa weledi, wakati alipokuwa Kamishna wa Polisi Zanzibar.