Zenj FM

Chama Cha Wanasheria Zanzibar kimetakiwa kupaza sauti dhidi ya vitendo vya uvunjaji wa sheria.

29 October 2024, 6:41 pm

Makamu wa Kwanza wa Rais Othman Masoud Othman,akimkabidhi zawadi wakili Hassan Kijogoo wakati akifunguwa mkutano mkuu wa mwaka wa chama hicho uliofanyika katika hoteli ya verde mjini Zanzibar.

Na Mary Julius.

Makamu wa Kwanza wa Rais Othman Masoud Othman, amekitaka chama cha wanasheria Zanzibar kiwe mstari wa mbele kupaza sauti na kuchukua hatua stahiki dhidi ya vitendo vya uvunjaji wa sheria na katiba vinapojitokeza.

Ameyasema hayo wakati akifunguwa mkutano mkuu wa mwaka wa chama hicho uliofanyika katika hoteli ya verde mjini Zanzibar

Akizungumzia uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwakani amesema uchaguzi sio jambo la chama cha siasa bali ni haki ya wananchi ya kikatiba na kila mwananchi anapaswa kupewa haki ya kuchagua au kuchaguliwa.

Sauti ya Makamu wa Kwanza wa Rais Othman Masoud Othman.

Naye aliyekuwa Rais wa Chama cha Wanasheria Masoud Rukazibwa, amesema chama chao kinakabiliwa na changamoto nyingi ikiwemo mawakili kutengwa katika kazi za kusimamia mikataba ya miradi ya maendeleo na kazi hiyo kufanywa na wanasheria wa serikali.

Amesema wanakabiliwa na changamoto ya upungufu wa rasilimali hususan katika maeneo ya vijijini ambako huduma za kijijini bado zinahitaji sana.

Aidha amelalamikia hatua za wanasheria wa serikali kufanya kazi za uwakili kwa kutoza gharama ndogo jambo linalochangia kuharibu kazi ya uwakili hasa kwa vile wanasheria waserikali hawapaswi kufanya kazi za uwakili wa waaina hiyo.

Sauti ya Rais wa Chama cha Wanasheria Masoud Rukazibwa,
Makamu wa Kwanza wa Rais Othman Masoud Othman na Waziri wa Katiba, Sheria na Utawala Bora, Haroun Ali Suleiman katika mkutano mkuu wa mwaka wa Chama cha Wanasheria uliofanyika katika hoteli ya verde mjini Zanzibar.

Kwa upande wake Waziri wa Katiba, Sheria na Utawala Bora, Haroun Ali Suleiman amesema serikali inaendelea na kazi kubwa ya kuimarisha serikali ya umoja wa kitaifa na kuwataka wanasheria kuunga mkono juhudi hizo ili kujenga umoja wa kitaifa kwa wananchi wa Zanzibar.

Aidha Waziri, Haroun amewataka wanasheria kufuata maadili ya kazi zao kwa kutenda haki na kujenga imani na serikali na hakuna tatizo katika kuikosoa ama kuishauri serikali.

Sauti ya Waziri wa Katiba, Sheria na Utawala Bora, Haroun Ali Suleiman.

Chama hicho kimefanya uchaguzi mkuu na kumchagua Joseph Magazi kuwa rais wa chama hicho baada ya alikuwa rais kumaliza muda muda wake.