Marufuku kupiga muziki baa kama huna Sound Proof Zanzibar
18 October 2024, 3:41 pm
Na Sallhiya Hamad
Baraza la Sanaa, Sensa, Filamu na Utamaduni Zanzibar, limezuia upigaji wa muziki katika baa zote za Zanzibar ambazo hazina sehemu maalumu ya kuzuia sauti (sound proof) ili kuepusha usumbufu kwa jamii.
Akitoa taarifa kwa vyombo vya habari , Katibu Mtendaji wa Baraza hilo Chum Juma Chum, amesema hatua hiyo imekuja baada ya kupata maalamiko kutoka kwa jamii juu ya upigwaji huo wa muziki na kusababisha kero.
Amesema baraza limesitisha utoaji wa leseni za muziki kwa kumbi za baa hadi pale zitakapokidhi vigezo na masharti ikiwemo sehemu ya kudhibiti sauti.
Hata hivyo baraza linaendelea kufanya ziara ya ukaguzi katika maeneo yote ya kumbi za burudani kwa lengo la kudhibiti athari zinazotokana na kelele za muziki kwa jamii.
Aidha amezitaka taasisi na jamii kwa ujumla kufuata sheria na taratibu za baraza hilo ikiwemo ukataji wa leseni ili kuepusha kufungiwa na endapo watakiuka sheria hizo hatua kali za kisheria atachukuliwa dhidi yao.
Akizungumzia kuhusu Shughuli za kijamii amesema utaratibu utaendelea kama kawaida kwa kufuata maelekezo ya vibali vinavyotolewa na masheha wa maeneo husika.
Nae Mrajis wa baraza hilo, Abdillahi Ramadhan Nyonje, amesema Baraza kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama watafanya zoezi la ukaguzi wa baa zote ili kudhibiti vitendo vya uhalifu vinavyoweza kujitokeza katika baa hizo.