Vikoba vyawa mkombozi kwa wanawake wilayani Kyela
17 September 2023, 15:37
Vikoba wilayani Kyela vimetajwa kuwa chanzo kikuu cha kuinua uchumi kwa wanawake na kupelekea kujikwamua kiuchumi na kuwa tegemezi kwenye familia.
Na Secilia Mkini
Imeelezwa kuwa vikoba kwa wanawake ni njia mojawapo inayoinua uchumi kwa wanawake kwani huwasaidia katika kuendesha shughuli mbalimbali za kimaendeleo ikiwemo biashara.
Hayo yameelezwa na mtaalam wa masuala ya kiuchumi Dkt. Leny Kasionga wakati wa mahojiano maalum na Redio Keifo Fm na kusema kuwa vikoba kwa wanawake ni njia mojawapo inayosaidia katika malezi ya familia.
Sambamba na hayo ameeleza changamoto wanazokumbana nazo wanawake hao katika kuendesha vikoba ikiwemo msongo wa mawazo jambo linalohatarisha saikolojia ya wanawake wengi.
Kwa upande wao baadhi ya wanawake wanaojihusisha na vikoba wameeleza faida wanazozipata kutokana na vikoba ikiwemo kuepukana na utegemezi kwa wenza wao.
Licha ya faida inayopatikana katika vikoba wanawake hao wameeleza changamoto wanayoipata pindi inapotokea wanakopa katika vikoba vyao ikiwemo suala la kushindwa kurudisha mikopo kwa wakati.
Vikoba huendeshwa kwa njia ya uwekezaji wa fedha na ukopeshwaji kutokana na hisa za mshiriki ambapo wengi wao huendesha shughuli mbalimbali kutokana na uwekezaji huo unaofanywa kila baada ya muda waliokubaliana.