Ibasa washerehekea Krismasi, mwaka mpya na wenye ualbino Kyela
27 December 2023, 21:30
Vifaa tiba pamoja na vifaa vya shule vyenye thamani ya shilingi milioni nne na laki tisa vimetolewa na umoja wa wanakyela waishio sehemu mbalimbali maarufu Ibasa katika kituo cha afya Njisi na sekaondari mpya ya njisi iliyoko kata ya Njisi hapa wilayani Kyela.
Na Nsangatii Mwakipesile
Wakati watanzania wakiungana na watu wengine duniani kusherehekea sikukuu za Krismasi na Mwaka mpya umoja wa wanakyela waishio sehemu mbalimbali maarufu Ibasa wameungana na watu wenye ualbino na kukabidhi vifaa tiba katika kituo cha afya cha njisi.
Hayo yamejiri mapema leo wakati umoja huo ukiwa hapa wilayani Kyela na kuendelea na shughuli mbalimbali za kijamii ikiwemo kuungana na watu wengine katika kuwafariji wenye shida mbalimbali.
Akizungumza kwa niaba ya mwenyekiti wakati wa shughuli za kukabidhi vifaa tiba katika kituo cha afya cha Njisi Vanesa Ngesienge mwenyekiti wa jamii Ibasa amesema umekuwa ni utamaduni wao kila ifikapo mwisho wa mwaka kukaa na watu wenye shida mbalimbali ikiwemo masuala mazima ya afya na elimu.
Ameongeza kuwa vifaa hivyo vilivyotolewa vinathamani ya shilingi milioni nne na laki tisa fedha zilizotokana na wao wenyewe kuchangishana na wenzao kutoka sehemu mbalimbali.
Kwa upande wa mganga mfawidhi wa kituo cha afya njisi Jonson Mganyizi akizungumza kwa niaba ya mganga mkuu wa wilaya ya Kyela amewashukuru wanakyela hao kwa misaada hiyo waliyoitoa kwa kituo hicho.
Naye diwani wa kata ya njisi Omary Mwinjuma ameungana na mganga mfawidhi kutoa shukrani kwa wanaibasa kwa msaada walioutoa kwa wananchi wake huku akisema kufanya hivyo ni kuunga mkono jitihada za serikali ya awamu ya sita chini ya raisi kipenzi cha watanzania Samia Suluhu Hasan
Akizungumza kwa niaba ya watu wenye ualbino mwenyekiti wa TASI wilayani Kyela Bwigane Mwamasangula amepongeza sana watu wa ibasa na kuwaomba kuendelea kuwakumbuka kwani bado wanamahitaji mengi muhimu wanayoyahitaji kama watu wenye ualbino hapa wilayani Kyela
Umoja wa wanakyela waishio sehemu mbalimbali wamekuwa na utaratibu wa kukutana kila mwisho wa mwaka na kutoa misaada kwa wananchi wenye uhitaji mbalimbali kama sehemu ya wao kurudisha nyambani ambapo leo wametoa vifaatiba vyenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni nne za kitanzania.