Mwamengo: Waislamu bebeni jukumu la malezi hakuna mtoto asiye na wazazi
4 December 2023, 09:39
Maadhimisho ya kuzaliwa kwa Mtume Muhammad Wilaya ya Kyela yamefanyika katika msikiti wa Wilaya na kuhudhuriwa na madau wa maendeleo mhandisi Baraka Mwamengo.
Na Masoud Maulid
Zaidi ya shilingi milioni nne zimepatikana katika harambee ya ununuzi wa kiwanja cha kujenga Msikiti Kata ya Nkuyu,harambee iliyofanyika kwenye Maadhimisho ya kuzaliwa kwa Mtume Muhammad Wilaya ya Kyela desemba 2, 2023.
Akizungumza kwenye maadhimisho hayo Kadhi wa mkoa wa mbeya Hasan Mbaliza amesema kwa mujibu wa baraza kuu la waislamu tanzania bakwata sherehe za kuadhimisha kuzaliwa kwa mtume Muhammad kwa ngazi ya wilaya zinafanyika baada ya kumalizika ngazi ya Kitaifa na Mkoa hivyo amewapongeza viongozi wa wilaya ya kyela kwa kufuata utaratibu huo.
Mbalazi ameongeza kuwa kukusanyika Waislamu na wasiokuwa Waislamu kwa ajili ya Maadhisho ya kuzaliwa Mtume kunafaida kubwa,ikiwa ni pamoja na kujua historia ya Mtume tangu kuzaliwa kwake hadi kifo pamoja na kujua kazi muhimu alizotumwa na mwenyezi Mungu, pamoja na kueneza mambo ya imani ya kumjua Mungu mmoja na kuacha kufanya ibada ya Masanamu.
Katika Maadhimisho ya mwaka huu Kadhi wa Mkoa kwa niaba ya Shekhe wa Mkoa wa Mbeya amewataka Waislamu na wasiokuwa Waislamu kuzingatia swala la malezi kwa Watoto kutokana na hali ya maadili inavyozidi kuporomoka siku hadi siku hasa ndoa zinapovunjika, Wanaume wengi wamekuwa wakiwatelekezea wanawake Watoto na kukwepa jukumu la Malezi.
Katika risala kwa Mgeni rasmi katika Maadhimisho hayo iliyosomwa na Katibu wa Bakwata Wilaya ya Kyela Juma Yatera,Waislamu wameeleza changamoto ya kuuendeleza Usilamu Wilaya ya Kyela ikiwemo kukosekana kwa nyumba za ibada katika baadhi ya maeneo,kukosekana miundombinu ya maji na umeme,hivyo kumuomba Mgeni rasmi kuendesha harambee itakayowezesha ununuzi wa kiwanja cha kujenga Msikiti chenye thamani ya Shilingi milioni arobaini na tano.
Kwa upande wake mgeni rasmi Baraka Mwamengo ambaye ni Mkurugenzi wa Kampuni ya Ujenzi wa Barabara BASAI General Supplies LTD,amewapongeza Waislamu kwa kuadhimisha kuzaliwa Mtume Muhammadi pamoja na upendo waliouonesha kumualika kuhudhuria kwenye sherehe hiyo,ambapo amewasihi Waumini wa dini ya kiislamu kila mmoja kulibeba jukumu la malezi kwa watoto kwakuwa hakuna mtoto asiyekuwa na wazazi.
Akijibu risala Mgeni rasmi amesema kwakuwa nyumba inayotarajiwa kujengwa ni nyumba ya Mwenyezingu ambayo itasaida Waislamu kufanya ibada pamoja watoto kusoma Madrasa,hivyo amekubari kuchangia kiasi cha shilingi Milioni tatu,huku na zaidi ya Milioni moja zikipatikana kwa njia ya harambee kwa Waislamu waliohudhuria maadhimisho hayo.
Mtume Muhammadi alizaliwa siku ya Jumatatu Mwezi kumi na mbili Mfungo sita Mwaka wa tembo,hivyo Waislamu huadhimisha kuzaliwa kwake kila mwaka mwezi wa mfungo sita.