Karagwe FM

Bei ya nyama yapanda ghafla katika mji wa Bunazi Missenyi

4 January 2025, 2:38 pm

Moja ya maduka ya nyama yaliyobandikwa bei mpya ya nyama katika mji wa Bunazi. Picha na Respicius John
Mkoa wa Kagera ni moja ya mikoa yenye kiwango kikubwa cha mifugo ikiwemo ng’ombe jambo linalotoa tumaini kwa wananchi kuwa kitoweo aina ya nyama na mazao mengine ya mifugo yangeuzwa kwa bei nafuu lakini hali ni tofauti

Na Respicius John, Missenyi Kagera

Baadhi ya wakazi wa mji mdogo wa Bunazi wilayani Missenyi wamelalamikia ongezeko la bei ya nyama ya ng’ombe iliyopanda holela kutoka shilingi elfu 8 mpaka shilingi elfu kumi kwa kipindi cha takribani miezi minne.

Mmoja wa wafanyabiashara ya nyama mjini Bunazi bw. Swidiq Mustafa. Picha na Respicius John

Wakiongea na Radio Karagwe FM kwa nyakati tofauti baadhi ya watumiaji wa nyama katika mji mdogo wa Bunazi wamelalamikia ongezeko hilo wakidai kuwa haliendani na uhalisia wa maisha yao na kipato chao. Hata hivyo baadhi ya wafanyabiashara ya nyama mjini hapo akiwemo Swidiq Mustafa wamedai kuwa kufungwa kwa minada ya ng’ombe na ongezeko la kodi wakati wa ununuzi wa ng’ombe kumechangia hali hiyo

Sauti ya bw. Muktaru Hassan na Swidiq Mustafa wakizungumzia tatizo la bei ya nyama. Picha na Respicius John
Bw. Mukhtaru Hassan, mkazi wa Bunazi. Picha na Respicius John

Diwani wa kata ya Kasambya Yusuph Ahmada Mzumbe amekiri uwepo wa changamoto hiyo mjini Bunazi na kuahidi kufuatilia chanzo cha tatizo la upandishaji wa bei za kitoweo hicho  

Sauti ya Diwani wa kata ya Kassambya wilaya ya Missenyi bw. Yusuph Ahmada Mzumbe
Kaimu mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya Missenyi wakili Serafina Rwegasira

Kuhusu suala hilo kaimu mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Missenyi wakili Serafina Rwegasira ambaye pia ndiye mwanasheria wa halmashauri hiyo amesema kuwa halmashauri haina mamlaka ya kupanga bei ya bidhaa hiyo bali wafanyabiashara wenyewe hupanga bei kulingana na upatikanaji wa soko na bidhaa husika.

Pamoja na hayo amekanusha suala la kupanda ushuru kama lilivyotajwa na wafanyabiashara wa nyama akisisitiza kuwa viwango vya ushuru vilivyopo ni vya muda mrefu

Sauti ya kaimu mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Missenyi wakili Serafina Rwegasira