DED Missenyi atumia milioni 2 kwa waliokatika miguu kwa ugonjwa wa ajabu
2 January 2025, 11:09 am
Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya Missenyi mkoani Kagera wakili John Paul Wanga ameguswa na changamoto ya watu sita wenye ulemavu utokanao na ugonjwa wa ajabu na kuwashika mkono katika kijiji cha Lukuba A wilayani humo
Na Respicius John, Missenyi Kagera
Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya Missenyi mkoani Kagera ametoa msaada wa vyakula na mahitaji mengine yenye thamani ya shilingi milioni 2 kwa familia yenye watu 6 waliokatika miguu kwa ugonjwa wa ajabu
Msaada huo umekabidhiwa kwa watu hao Jumatano tarehe 1 Januari 2025 katika kitongoji cha Lukuba A, kijiji cha Igayaza kata ya Nsunga nyumbani kwa bi Hadija Omary aliyekatika miguu yeye na mtoto wake mmoja, wajukuu watatu pamoja na kitukuu chake
Akikabidhi msaada huo kwa niaba ya mkuu wa wilaya ya Missenyi katibu tawala wa wilaya bi Mwanaidi Mang’uro amempongeza mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Missenyi wakili John Paulo Wanga kwa kuona umuhimu wa kutoa mkono wa sikukuu ya mwaka mpya kwa familia hiyo yenye uhitaji inayoishi katika mazingira magumu yaliyosababishwa na ugonjwa wa ajabu wa kukatika miguu
Aidha Bi Mang’uro amewatia moyo wanafamilia kwa changamoto ya ulemavu inayokabili pia akawashauri kuwaombea watu wote wanaowapa misaada ya hali na mali ili kuwezesha usitawi wa maisha yao pia akatumia fursa hiyo kuwaomba watu wengine kusaidia familia hiyo yenye uhitaji
Akitoa neno la shukrani bi Amina Omary amemshukuru Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya Missenyi na serikali kwa ujumla kwa msaada mkubwa wanaoendelea kutoa pia akamuomba Rais wa Tanzania Dr Samia Suluhu Hassan na wadau wengine kumsaidia kwakuwa anateseka kuhudumia familia ya watu sita waliokatika miguu ambao kwasasa wanahitaji miguu bandia,matibabu na mahitaji mengine ya kibinadamu huku diwani wa kata ya Nsunga Jamary Suleiman Rulengwa akimshukuru mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya kwa kuijali familia hiyo