Wafanyakazi Tume ya Uchaguzi Zanzibar watakiwa kufanya kazi kwa mashirikiano
15 December 2023, 3:40 pm
Na Mary Julius.
Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar George Joseph Kazi amewataka wafanyakazi wa tume hiyo kuendelea kufanya kazi kwa mashirikiano na kutoa michango katika jumuiya za kikanda.
Mwenyekiti ameyasema hayo katika hafla ya kukabidhi tuzo ya mjumbe aliyeshiriki kuandaa katiba ya Umoja wa Tume za Uchaguzi za Nchi za Kusini mwa Afrika ECF- SADC na kuweka saini katika katiba hiyo Marehemu Hassan Saidi Mzee pamoja na kukabidhi tuzo ya Tume ya Uchaguzi Zanzibar, hafla iliyo fanyika katika ofisi za Tume hiyo Zanzibar.
Jaji George, amesema kupokelewa kwa tuzo kumeleta heshima kwa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar kwa kuonyesha mchango wake kwa umoja huo ikiwa ni ishara ya kuwa kuna kazi kubwa imefanyika.
Kwa Upande Wake Mkurugenzi Wa Tume ya Uchaguzi Thabit Idarous Faina amesema umoja wa Tume za Uchaguzi za Nchi za Kusini mwa Afrika ECF-SADC unakabiliwa na changamoto mbali mbali ikiwemo kutofautiana kwa miundo ya kitaasisi na mifumo ya uchaguzi miongoni mwa nchi wanachama katika kuendesha chaguzi za nchi husika pamoja na ukosefu wa fedha na watendeaji katika kuendeleza shughuli za umoja huo.
Akitoa maelezo ya tuzo hizo Mkuu wa Kurugenzi ya Mipango,Utumishi na Utawala Saadun Ahmed Khamis amesema umoja huo umetoa tuzo ya heshima kwa Marehemu Hassan Saidi Mzee ikiwa ni kumbukumbu na shukrani ya kutambua mchango wake alioutoa wakati wa uhai wake katika kuimarisha masuala ya kidemokrasia na kuendesha uchaguzi.
Akizungumza mara baada ya kukabidhiwa tuzo hiyo kwa niaba ya familiya ya marehemu Hassan Said Mzee, Jaji Saidi Hassan Said amesema wamefarijika kwa kupokea tuzo hiyo ambayo unaonyesha kuthamini juhudi za marehemu alizo zifanya wakati wa uhai wake
Umoja wa Tume za Uchaguzi za Nchi za Kusini mwa Afirika uanajumuisha Tume za Uchaguzi zilizopo katika Nchi za SADC umoja huo unawanachama kumi na tano ambazo ni Angola Botswana, Drc Kongo ,Eswatini Lesotho, Malawi, Mauritius Mozambique, Namibia, South Afrika ,Seychelles, Tanzania ,Zambiam Zanzibar Na Zimbabwe.