Zenj FM

Polisi watakiwa kutumia mafunzo kupambana na changamoto za usalama

29 March 2025, 6:30 pm

Naibu Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Zanzibar, Naibu Kamishna wa Polisi DCP Zuber Chembera.

Na Omar Hassan.

Naibu Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Zanzibar, Naibu Kamishna wa Polisi DCP Zuber Chembera amewataka Maafisa na Wakaguzi wa Polisi kutumia mafunzo mbalimbali wanayopatiwa kuondoa changamoto za kiusalama zilizopo kwenye jamii na kupunguza malalamiko ya wananchi dhidi ya utendaji wa Jeshi la Polisi.
Akifunga Mafunzo ya Utayari kwa Maafisa na Wakaguzi wa Makao Makuu ya Polisi Kamisheni ya Zanzibar na Mkoa wa Mjini Magharibi huko Kambi ya Kikosi cha Kutuliza Ghasia DCP Chembera ameyataja makosa ambayo yamekuwa yakiongezeka na kuwa changamoto kubwa kwa jamii kuwa ni pamoja na Mauaji, wizi wa pikipiki, wizi wa mifugo, makosa yatokanayo na vitendo vya udhalilishaji na makosa ya usalama barabarani.

Sauti ya Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Zanzibar, Naibu Kamishna wa Polisi DCP Zuber Chembera.

Nae Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Richard Mchomvu amesema mafunzo yanayoendelea kutolewa kwa Maafisa na Wakaguzi ni muhimu katika kuwajenga na kuwasaidia kufanya kazi kwa weledi katika maeneo yao ya kazi.
Kwa upande wake Mkuu wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia Mkoa wa Mjini Magharibi, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Elisante Makiko Mmari amesema miongoni mwa masomo yaliyofundishwa ni Uzalendo, mikakati ya kuimarisha ulinzi, utatuzi wa migogoro, uongozi na maadili.