RC Salama atoa wito wa kutunza miti ya mikoko kupambana na athari za tabia nchi
11 December 2024, 4:14 pm
Na Is-haka Mohammed.
Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba Salama Mbarouk Khatibu amewasisitiza wananchi wanaoishi pembezoni mwa bahari kuendelea kuilinda miti ya mikoko na kupanda katika maeneo iliyotoweka ili kuepukana na athari kubwa zaidi za mabadiliko ya tabia nchi.
R.C Salama ametoa msisitizo huo wakati akizungumza na wananchi katika hafla ya upandaji wa miti ya mikoko huko Likoni kojani kwa ushirikiano wa Jumuiya ya Hifadhi ya Misitu wa Jamii Pemba(Pemba Community Forest na Jeshi la Wananchi wa Tanzania ikiwa ni maadhimisho ya siku ya Uhuru wa Tanganyika.
Amesema kuendelea kukata miti ya mikoko na mengine kutaongeza athari za kimazingira katika maeneo yao ikiwemo maji ya bahari kuingia kwenye mashamba na makaazi yao.
Mkurugenzi wa Jumuiya ya Pemba Community Forest Mbarouk Mussa amesema athari mbali mbali za ukataji wa miti ya mikoko kwa shughuli mbali mbali za kijamii zimekuwa zikijitokeza katika maeneo tofauti huku Jumuiya hiyo ikiendelea kutoa elimu kwa jamii.
Akitoa salama za Jeshi la Wananchi Kambi za Pemba Mkuu wa Kikosi cha 151 cha JWTZ Chaku Msuya amesema ushiriki wao katika upandaji wa mikoko ni kushirikiana na jamii katika kusheherekea miaka 63 ya Uhuru wa Tanganyika.
Zaidi ya mikoko laki moja na elfu arobaini na tano na mia tatu (145,300) ilipangwa katika eneo hilo ambapo mbali na jeshi la wanajeshi wa JWTZ pia vikosi vyengine vya ulinzi na usalama vilishirikiana na wananchi na maofisa mbali mbali wa serikali katika zoezi hilo.