Zenj FM

Kashfa za maneno, vitendo zinavyotesa wanawake kuwa viongozi Zanzibar

26 November 2024, 7:31 pm

Naibu Katibu wa Haki za Binadamu kutoka Chama cha ACT-Wazalendo Pavu Abdallah.

Na Ivan Mapunda.

Sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022 inaonesha Zanzibar ina watu 1,889,773 kati ya hao wanaumme ni 915 ,492 na wanawake ni 974 ,281 hii inamaanisha kwamba wanawake ni asilimia 51.6 ya wakazi wote Zanzibar.

Licha ya wanawake kuwa wengi bado kumekuwa na upungufu wa wanawake kushiriki katika kushika nafasi za uongozi katika ngazi za maamuzi na nafasi za chama kutokana na vikwazo tofauti vikiwemo kashfa ya maneno na vitendo wakati wa kujitoa kuingia kwenye uchaguzi au hata kwenye kampeni.

Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake tanzania upande wa Zanzibar –TAMWA-Z .Katika ripoti yao june 2024 inayohusu uchambuzi wa ukatili dhidi ya wanawake katika vyama vya siasa Zanzibar imeeleza kuwa washiriki wa utafiti walirekodi visa vya ukatili wa kijinsia ni asilimia 21.88% na hakukuwa taarifa za kuripoti matukio hayo.Wanaharakati wa masuala ya kijinsia nchini wanasema vipo vikwazo vingi vinavyokwamisha jitihada za wanawake kuwa viongozi.

Mkurugenzi wa Haki za Binadamu na Sheria katika Chama Cha Wananchi – CUF Nadhira Ali Haji amesema rushwa, kashfa, mila potofu na udhalilishaji wa kijinsia ni miongoni mwa vikwazo vya kutofikia malengo ya kushiriki katika uchaguzi kuanzia kweny vyama hadi katika vyombo vya maamuzi.

   “Uchaguzi wa mwaka 2015 niligombania uwakilishi Jimbo la Mfenesini kupitia Chama Cha Wananchi CUF lakini jina langu halikurudi lilikatwa kwa sababu niliolewa na mume ambaye alikua ni mwanachama wa Chama Cha Mapinduzi- CCM  nilipambana kadri ya uwezo wangu lakini ilinirudisha nyuma sana.” Amesema Nadhira  huku maneno mabaya ndio yalimvuja zaidi moyo.”Nilitukanwa kiasi cha kuitwa majina mabaya na kutokuuziwa vitu dukani pale chama kilipogawanyika na nilipokubali kuunga mkono Chama Cha CUF, hata hivyo sikukata tamaa niliendelea kupambana na nikaungwa mkono familia yangu. Namshukuru mama yangu aliinuka kueleza kuwa nastahili,” Amemaliza Nadhira huku akionesha ujasiri juu ya kadhio iliyomkuta.

Maneno ya kashfa kwa wanawake wakati wa uchaguzi ni suala linaloumiza zaidi wanawake akiwemo Pavu Abdallah kutoka Mkoa wa Kaskazini Unguja amabye ni Naibu Katibu wa Haki za Binadamu kutoka ACT-WAZALENDO, amesema bado mifumo iliyokuwepo nchini sio rafiki kumuwezesha mwanamke kuwa kiongozi jasiri.”Utashangaa kipindi cha uchaguzi mwanamke anakuwa wa kwanza kutukanwa ,kupewashutuma na kutolewa udhaifu  wake pamoja na maneno yasiofaa “ .

Zipo taasisi ambazo zinajikita kuwasaidia wanawake wanasiasa na wale amabao wataka kuingia kwenye siasa kama Idara ya Taasis ya  Umoja wa Wanawake Tanzania , Salma Omar Said ni Katibu wa Idara hio  hapa Zanzibar amesema bado kuna safari ndefu ya kuhakikisha wanawake wanaheshimiwa wanapowania uongozi. “Licha ya kupambana usiku na mchana bado misukosuko ikiwamo kutukanwa, kudhalilishwa na kudhihakiwa imekuwa kikwazo kwa mwanamke kupata nafasi za uongozi.” Amesema Salma huku akiendelea kusema kuwa pia rushwa ya ngono ni moja ya kikwazo  kwa baadhi ya wanaume ambao wapo kwenye nafasi pindi unampomfuata kwa ajili ya usaidizi.

Wanaharakati wa masuala ya wanawake ni sehemu ya mapambano ya kuwasaidia na  kuwatetea,Fathya Zaharan ni mwanaharakati na mwanachama wa Chama Cha ACT WAZALENDO amesema wamepitia madhila na changamoto kadhaa katika harakati za siasa na kwa miaka kadhaa iliyopita ikiwemo kudhalilishwa kwa kuvuliwa nguo  na askari wanaume pamoja na kushikwashikwa. “baada ya kufika jela wakati tunapelekwa sehemu ya wanawake walitoka watoto wadogo kumi na kuanza kutukamata matiti,makalio na kufika ndani tuliliazimishwa kuvua nguo mbele ya askari wanaume. “

Bi fathya ameiomba serikali kusimamia taasisi zake kwa kufanya   kazi kwa kufuata misingi sheria na kanuni na miongozo inavyosema ili kuweza kuondoa vitendo vya udhalilishaji  nchini.

Chama cha Mapinduzi – CCM kupitia Katibu wa Kamati Maalum ya -NEC,Idara ya Itikadi,Uenezi na Mafunzo Khamis Mbeto khamis amesema CCM inaendelea kuwajengea uwezo wanawake wa kujiamini kusimama katika majukwaa na kugombania nafasi mbali mbali sawa na wanaume“ Jukumu kubwa la kuanda viongozi tumewapa jumuiya zetu  za  umoja wa vijana  na umoja wa  wanawake  kwa kufanya sema za uongozi  ili  kuwajengea wanawake uwezo , kuwatoa  hofu  na kujiamini “

Amesema pia  Chama cha Mapinduzi CCM kitaendelea kuwasimamia na kuwabeba wanawake na kuwaandaa kisaikolojia kukabiliana na vitisho,kashfa  ili isiwe sababu ya wao kurudi nyuma katika kugombania nafasi za uongozi

“wanawake wasivunjike moyo wataambiwa maneno mengi yasiofaa na kuitwa majina mabaya   endeleeni  kujiamini na  kujitokeza kugombania  nafasi mbali mbali  sisi kama ccm tutaendelea kuwabeba na kuwasimamia “

Mkurugenzi Jumuiya ya wanasheria wanawake Zanzibar ZAFELA, Jamila Mahamoud Juma amesema katika watu ambao walikuwa  wanalilia na kutamani kuona sera na  sheria zinalazimisha vyama siasa kuwa na sera ya jinsi ni sisi wanasheria maana kuwa na sera hizo kutuonyesha uwiano  wa usawa wa kijinsia ili kuondoa changamoto zote za udhalilishaji.”Kuwepo kwa sheria ya mpya ya uchaguzi mwaka 2024 itasaidia kupunguza na kuondoa vitendo vya udhalilishaji  na maneno ya kashfa wa wagombea ambavyo zaidi inawathiri wanawake kushiriki vizuri katika nafasi za uongozi na pia walipata hofu. ” Amesema Jamili huku akiongeza kuwa “ZAFELA moja  kazi yetu kuhakikisha kwamba jamii inapata msaada wa kisheria na  tumeomba  kuwa waangalizi katika uchaguzi wa mwaka 2025 ili kuangalia ushirikishwaji na ushiriki wa wanawake katika uchaguzi na kuona wanawake wanapata haki zao na hawavunjiwi heshima zao”. Amesema Jamila.

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na ile ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania imesaini mikataba mbalimbali ya kimataifa kama mkataba wa CEDAW ulioanzishwa mwaka 1979 ukiwa na  lengo la kupinga aina zote za udhalilishaji dhidi ya wanawake,itifaki ya SADC  ya mwaka 2008 na itifaki ya maputo ya mwaka 2003.