Zenj FM

SMZ yaimarisha mazingira na miundombinu ya skuli

10 October 2024, 2:35 pm

Mkuu wa Wilaya ya Magharibi B ambae Pia ni kaimu Mkuu wa Wilaya ya Magharibi A Hamida Mussa Khamis akizungumza katika ukaguzi wa majengo mawili ya vyoo katika Skuli ya Msingi Chunga ikiwa ni Shamra shamra za Kutimiza miaka 8 ya kuanzishwa kwa Baraza la Manispaa Magharibi A.

Na Mary Julius

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kuimarisha mazingira na miundombinu ya Skuli pamoja na kuweka huduma mbali mbali za kibinaadam katika Skuli hizo ili wanafunzi waweze kusoma katika mazingira bora.

Akizungumza katika ukaguzi wa majengo mawili ya vyoo katika Skuli ya Msingi Chunga ikiwa ni Shamra shamra za Kutimiza miaka 8 ya kuanzishwa kwa Baraza la Manispaa Magharibi A Mkuu wa Wilaya ya Magharibi B ambae Pia ni kaimu Mkuu wa Wilaya ya Magharibi A Hamida Mussa Khamis Amesema lengo la Serikali ni kuweka mazingira wezeshi kwa wanafunzi kuweza kujifunza na kuimarisha kiwango cha ufauli.

Amesema serikali inampango wa kujenga Skuli ya Ghorofa katika eneo la Skuli ya Msingi Chunga jambo ambalo litatowa fursa kwa wanafunzi kujifunza katika madarasa bora na ya kisasa hivyo amewaomba wazazi na walezi kuendelea kuunga mkono juhudi hizo za serikali katika kuwapatia elimu watoto wao.

Aidha Hamida amepongeza wazo la kuweka chumba maalum kwa wanafunzi wa kike ambacho wataweza kukitumia katika masuala yao binafsi jambo ambalo litaweza kuwapa nafasi na uhuru wa kuendelea na masomo muda wote.

Sauti ya Mkuu wa Wilaya ya Magharibi B Hamida Mussa Khamis.

Mkurugenzi wa Manispaa Magharibi A Mbaraka Said Hasuni amesema katika kipindi cha miaka nane tokea kuanzishwa Manisapaa hiyo wameweza kupiga hatua kubwa katika kutoa huduma kwa wananchi na wanaendelea na ujenzi wa miradi mbali mbali ya kimaendeleo ikiwemo ujenzi wa Vituo vya Daladala.

Sauti ya Mkurugenzi wa Manispaa Magharibi A Mbaraka Said Hasuni.

Jumla ya matundu 28 ya vyoo yamejengwa na Manispaa kupitia mfuko wa Diwani wa Wadi ya Mwera kwa Ufadhili wa Ubalozi wa Japan na umelenga kuondoa tatizo la upatikanaji wa huduma ya vyoo kwa wanafunzi wa skuli hiyo.