Uvinza FM
Uvinza FM
24 May 2026, 11:45 pm

Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) iliazishwa mwaka 2012 kwa kazi maalum ya kuleta maendeleo katika sekta ya kilimo nchini Tanzania.
Na. Abdunuru Shafii
Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) inaendesha semina kwa wamiliki na wahariri wa redio za kijamii ambazo ni redio wanachama wa Taasisi ya Maendeleo ya Redio za Jamii Tanzania – TADIO zipatazo 50 kutoka Tanzania Bara na Zanzibar, lengo kuu likiwa ni kukuza uelewa juu ya majukumu ya TADB pamoja na kuonesha fursa zinazopatikana katika benki hiyo.
Semina hiyo imefanyika katika Ukumbi wa Jengo la Mkandarasi Jijini Dodoma na kufunguliwa rasmi na Mkurugenzi wa Mipango, Ushauri na Mahusiano ya Taasisi TADB, ndugu Mkani Waziri, ambaye amesisitiza umuhimu wa vyombo vya habari katika kuelimisha jamii kuhusu mchango wa sekta ya fedha kwenye maendeleo ya kilimo na uchumi wa taifa kwa ujumla.

Mafunzo hayo yataimarisha ushirikiano kati ya vyombo vya habari vya kijamii na TADB katika kuhamasisha uelewa wa umma kuhusu fursa za uwezeshaji wa kifedha kwa wakulima, wafugaji, wavuvi na wadau wengine wa mnyororo wa thamani katika sekta ya kilimo.
Washiriki wamejengewa uwezo wa kuripoti masuala ya maendeleo ya sekta ya kilimo, fedha za kilimo, na nafasi ya taasisi za kifedha katika kuchochea ukuaji wa uchumi wa kilimo, ufugaji na uvuvi nchini.