Uvinza FM

Elimu ya madhara ya ukatili wa kijinsia shuleni

8 October 2026, 9:45 pm

Wanafunzi wakipokea zawadi kwa wawakilishi kutoka shirika la ENABEL.picha na France Alphonce

mradi huo unatekelezwa katika maeneo matatu makuu ambayo ni masuala ya kijinsia, elimu ya sekondari pamoja na ujuzi na ujasiriamali.

Na. Rehema Iddi

Shirika la Maendeleo la Ubelgiji (ENABEL), kwa kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma, limewazawadia wanafunzi waliofanya vizuri katika mashindano ya sanaa ya uchoraji yaliyolenga kuibua na kuelimisha jamii kuhusu athari za ukatili wa kijinsia, mimba za utotoni pamoja na ajira kwa watoto.

Zawadi hizo zimetolewa leo Septemba 7, 2026, katika Shule ya Sekondari Ntamya, iliyopo Kata ya Buhoro, kupitia Mradi wa Wezesha Binti unaotekelezwa na ENABEL kwa lengo la kupunguza ukatili wa kijinsia na mimba za utotoni, hususan kwa watoto wa kike.

Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Mratibu wa Mradi wa Wezesha Binti, Elizabeth Kimola, amesema mradi huo unatekelezwa katika maeneo matatu makuu ambayo ni masuala ya kijinsia, elimu ya sekondari pamoja na ujuzi na ujasiriamali. Amesema ushiriki wa vijana katika shughuli za mradi umekuwa mkubwa na umeleta matokeo chanya, huku sanaa ikiwa miongoni mwa njia zinazotumiwa kuwapa wanafunzi nafasi ya kujieleza na kuelimisha jamii kuhusu madhara ya ukatili.

Mratibu wa Mradi wa Wezesha Binti, Elizabeth Kimola akikabidhi za wadi kwa mwanafunzi alio ibua athari za ukatili.picha na France Alphonce.

Kwa upande wake, Mkuu wa Shule ya Sekondari Ntamya, Kojjo Tumbo, amesema Mradi wa Wezesha Binti umekuwa na mchango mkubwa kwa wanafunzi, hususan wale walio katika hatari ya kuacha shule kutokana na changamoto zinazohusiana na ukatili, kwani umewawezesha kutambua haki zao na kufahamu hatua wanazoweza kuchukua wanapokumbana na vitendo vya ukatili wa kijinsia.

Miongoni mwa wanafunzi walionufaika na mashindano hayo ni Joyce Jackson, ambaye amesema elimu waliyoipata kupitia Mradi wa Wezesha Binti imewasaidia kufahamu madhara ya ukatili na namna ya kujilinda ili waweze kutimiza ndoto zao.

ENABEL imepanga kuendelea na kampeni za kutoa elimu kuhusu madhara ya ukatili wa kijinsia katika kata tano za Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu ambazo ni Buhoro, Kagera Nkanda, Asante Nyerere, Kurugongo na Kwaga, kwa lengo la kuwafikia wanafunzi na jamii kwa ujumla.