Uvinza FM

Katubuka kujaa maji sasa basi

11 November 2026, 10:55 pm

Picha ya Meya wa Manispaa ya Kigoma Ujiji, Mhe. Mussa Maulid, akisaini mkataba. Picha na Rehema Iddi.

changamoto ya maji katika Bwawa la Katubuka imekuwa kero ya muda mrefu kwa wananchi na viongozi wa mkoa

Na. Abdunuru Shafii

Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma Ujiji imesaini nyongeza ya mkataba wa ujenzi wa mfereji maalumu wa kuondoa maji yanayotuama katika Bwawa la Katubuka na kuyaelekeza katika Ziwa Tanganyika kupitia eneo la Katonyanga, mradi unaotarajiwa kugharimu Shilingi bilioni tano na kukamilika ndani ya miezi mitatu.

Mkataba huo umesainiwa leo Novemba 11, 2026, katika Ukumbi wa Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma Ujiji, baina ya Halmashauri hiyo na kampuni za ASABHI CONTRACTOR LIMITED kwa kushirikiana na PIONEER BUILDERS LIMITED, katika hafla iliyohudhuriwa na Mkuu wa Wilaya ya Kigoma, Dkt. Rashid Chuachua amesema changamoto ya maji katika Bwawa la Katubuka imekuwa kero ya muda mrefu kwa wananchi na viongozi wa mkoa, hivyo amempongeza Mkurugenzi wa Manispaa kwa kuchukua hatua za haraka kutafuta suluhisho la kudumu na kusisitiza kuwa mkandarasi anapaswa kuanza kazi mara moja ili kupunguza madhara yanayoweza kusababishwa na maji hayo, hasa katika kipindi cha mvua.

sauti ya Mkuu wa Wilaya ya Kigoma Dkt. Rashid Chuachua

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma Ujiji, Eng. Juma Hamsini Seph, amesema kabla ya kuendelea na utekelezaji wa miradi hiyo, Halmashauri imeona umuhimu wa kufanya uhakiki wa fedha zilizolipwa kulinganisha na kazi zilizotekelezwa, akibainisha kuwa tathmini ya awali imeonesha kazi iliyofanyika ni kubwa kuliko kiasi cha fedha kilicholipwa.

sauti ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma Ujiji, Eng. Juma Hamsini Seph

Aidha, Meya wa Manispaa ya Kigoma Ujiji, Mhe. Mussa Maulid, amesema kusainiwa kwa mkataba huo ni hatua muhimu katika kutatua changamoto ya Bwawa la Katubuka, ambayo imekuwa ikiathiri wananchi na kuleta usumbufu katika Manispaa hiyo. Amesema utekelezaji wa mradi huo unalenga kurejesha matumaini kwa wananchi kupitia upatikanaji wa suluhisho la changamoto hiyo ya muda mrefu, akieleza kuwa hatua hiyo inaendana na dhamira ya Serikali ya kuhakikisha wananchi wanapata maendeleo na maisha bora.

sauti ya Meya wa Manispaa ya Kigoma Ujiji, Mhe. Mussa Maulid

Naye, mkandarasi wa mradi huo, Ibrahim Nyambacha, amesema wamepokea jukumu la ujenzi wa mfereji huo kwa uzalendo na watahakikisha wanakamilisha kazi ndani ya siku 90, sawa na miezi mitatu, ili kuwaondolea wananchi adha ya maji yanayotuama katika eneo hilo.

sauti ya mkandarasi wa mradi, Ibrahim Nyambacha