Uvinza FM

Mwenyekiti wa Kijiji cha Juhudi, Wilaya ya Kakonko jela miaka 40 kwa Rushwa

26 November 2026, 2:07 pm

Picha ya jengo la Mahakama ya wilaya ya kakonko.Pcha na Abdunuru Shafii

Mshtakiwa alikuwa anakabiliwa na makosa mawili (02) ambayo ni Uchepushaji pamoja na matumizi mabaya ya mamlaka kinyume na vifungu vya 29 na 31 vya Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Sura ya 329 Marejeo ya Mwaka 2023

Na.Rehema Iddi

Mwenyekiti wa Kijiji cha Juhudi, Wilaya ya Kakonko, Mkoa wa Kigoma Bw. Amos Hussein Kwigira (45), amehukumiwa kifungo cha miaka 40 jela baada ya kupatikana na hatia ya makosa mawili (2) ya Rushwa yaliyohusisha matumizi ya fedha za umma kiasi cha Shilingi 5,000,000 ambapo kila kosa lina adhabu ya miaka 20 jela.

Mahakama ya Wilaya Kakonko mnamo Novemba 25, 2026 mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Kakonko Mh. Ambilike Japhet Kyamba (SRM) limeamuriwa Shauri la Uhujumu Uchumi namba ECC.18335/2026 dhidi ya Mshtakiwa Bw. Amos Hussein Kwigira (45) ambaye ni Mwenyekiti wa Kijiji cha Juhudi katika Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko

Mshtakiwa alikuwa anakabiliwa na makosa mawili (02) ambayo ni Uchepushaji pamoja na matumizi mabaya ya mamlaka kinyume na vifungu vya 29 na 31 vya Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Sura ya 329 Marejeo ya Mwaka 2023 vikisomwa pamoja na Aya ya 21 ya Jedwali la kwanza na vifungu vya 57(1) na 61(2) vya Sheria ya Uhujumu Uchumi na Uhalifu wa Kupangwa Sura ya 200 Marejeo ya Mwaka 2023.

Mshtakiwa mnamo Mwezi Machi, 2026 akiwa maeneo ya kituo cha Mabasi Kakonko ndani ya Wilaya ya Kakonko Mkoa wa Kigoma alipokea fedha kiasi cha Tshs. 5,000,000 fedha za Kijiji cha Juhudi kutoka kwa Mfugaji na kukitumia kwa manufaa yake binafsi.

Shauri hilo liliendeshwa na Mwendesha Mashtaka wa Serikali Bw. Abdulrahim Omari ambapo aliwasilisha hoja na ushahidi katika kuthibitisha makosa yaliyokuwa yakimkabili mshtakiwa.

Hukumu hiyo ni sehemu ya juhudi za kuimarisha uwajibikaji na kulinda mali za umma, sambamba na kuhakikisha kuwa viongozi wa umma wanatekeleza dhamana walizopewa kwa kuzingatia sheria, uadilifu na misingi ya utumishi wa umma.