Uvinza FM
Uvinza FM
30 May 2026, 1:39 am

Tumelenga kuwajengea uwezo wananchi hususan wanawake na vijana juu ya usimamizi bora wa taka na matumizi yake katika shughuli za maendeleo.
Na. Rehema Iddi
Baadhi ya wananchi wa Wilaya ya Uvinza mkoani Kigoma wamepatiwa mafunzo kuhusu namna ya kubadili taka kuwa fursa ya kiuchumi huku wakihamasishwa kushiriki katika uhifadhi wa mazingira yanayozunguka Ziwa Tanganyika.
Mafunzo hayo yametolewa na Shirika la Catholic Relief Services (CRS) kwa kushirikiana na Caritas pamoja na wadau wengine wakiwemo Shirika la Jamii Integrated Development Initiative (JIDI), chini ya ufadhili wa Umoja wa Ulaya, yakilenga kuwajengea uwezo wananchi hususan wanawake na vijana juu ya usimamizi bora wa taka na matumizi yake katika shughuli za maendeleo.
Baadhi ya wananchi walioshiriki mafunzo hayo wamesema elimu waliyoipata imewasaidia kubadili mtazamo wao kuhusu taka, wakieleza kuwa awali waliziona kama uchafu usio na manufaa, lakini sasa wameelewa kuwa zinaweza kutumika kama chanzo cha kipato na ajira.
Kwa upande wao, maafisa mazingira kutoka kata mbalimbali za Wilaya ya Uvinza wamesema mafunzo hayo yamekuja kwa wakati muafaka kwani yatawasaidia kuendelea kutoa elimu kwa jamii kuhusu utunzaji wa mazingira, ukusanyaji sahihi wa taka pamoja na namna ya kuzitumia katika shughuli za uzalishaji mali.
Akizungumza kuhusu kampeni hiyo, Msemaji wa Shirika la JIDI lenye makao makuu jijini Dar es Salaam, Issack Kitururu, amesema kampeni ya “Taka ni Pesa” inalenga kubadili fikra na mtazamo wa wananchi ili waone taka kama rasilimali inayoweza kuchangia maendeleo ya kiuchumi badala ya kuziona kama uchafu unaopaswa kutupwa pekee.
Ameongeza kuwa kupitia kampeni hiyo, wananchi wanahamasishwa kushiriki kikamilifu katika shughuli za utunzaji mazingira sambamba na kujiongezea kipato kupitia urejelezaji wa taka na shughuli nyingine zinazotokana na usimamizi bora wa mazingira.