Uvinza FM
Uvinza FM
1 May 2026, 8:52 pm

sekta za umma na binafsi kuhakikisha haki na stahiki za wafanyakazi zinatekelezwa kwa wakati bila ubaguzi.
Na. Abdunuru Shafii
Maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani yamefanyika kimkoa katika Wilaya ya Uvinza, mkoani Kigoma, ambapo viongozi wa serikali, vyama vya wafanyakazi pamoja na wafanyakazi kutoka sekta mbalimbali wamekusanyika katika viwanja vya Shule ya Msingi Kachiringuro.
Akisoma risala kwa niaba ya Chama cha Wafanyakazi wa Serikali za Mitaa Tanzania (TALGWU) Mkoa wa Kigoma, Chama cha Wafanyakazi wa Serikali za Mitaa Tanzania (TALGWU) Mkoa wa Kigoma chama hicho, Johnson Muyombya, amesisitiza umuhimu wa waajiri katika sekta za umma na binafsi kuhakikisha haki na stahiki za wafanyakazi zinatekelezwa kwa wakati bila ubaguzi. Amesema kauli mbiu ya mwaka huu inalenga kuhamasisha uwajibikaji kwa pande zote waajiri na vyama vya wafanyakazi katika kulinda maslahi ya wafanyakazi kwa kuzingatia sheria za kazi zilizopo nchini.
Muyombya ameongeza kuwa utekelezaji sahihi wa sheria za kazi unachangia kujenga mazingira bora ya kufanyia kazi, kuongeza tija na kuimarisha mahusiano kati ya waajiri na wafanyakazi. Aidha, ametoa wito kwa wafanyakazi kote nchini kufanya kazi kwa juhudi, maarifa na uadilifu, huku akisisitiza umuhimu wa kupambana na rushwa katika maeneo ya kazi ili kulinda heshima ya utumishi wa umma na sekta binafsi.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Balozi Simon Sirro, amewataka waajiri na wafanyakazi kuzingatia uwiano wa haki na wajibu ili kuimarisha utendaji kazi na utoaji wa huduma kwa wananchi. Amesema kauli mbiu ya mwaka huu inaweka mkazo katika kulinda haki za wafanyakazi, kuboresha mazingira ya kazi na kuhakikisha ustawi wao, huku akibainisha kuwa waajiri wanapaswa kuzingatia sheria za kazi na kulipa stahiki kwa wakati ili kuongeza ari ya kazi.
Balozi Sirro pia amewatahadharisha watumishi dhidi ya uzembe na ukosefu wa nidhamu ya muda, hasa kwa wale wanaopangiwa vituo vya huduma vijijini lakini wanashindwa kutimiza majukumu yao ipasavyo. Amesisitiza kuwa haki haiwezi kutenganishwa na uwajibikaji, akiongeza kuwa serikali itaendelea kuboresha mifumo ya ufuatiliaji wa watumishi ili kuhakikisha huduma zinazotolewa kwa wananchi zinakuwa suluhisho la changamoto zao badala ya kuwa kero.