Uvinza FM

Walimu watakiwa kujipanga kwa mfumo mpya

1 May 2026, 12:57 am

Afisa Elimu Awali na Msingi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu, Bi. Elestina Chanafi akiongoza kikao cha Elimu ngazi ya Halmashauri (DEM) cha Divisheni ya Elimu Awali na Msingi Picha Na. Halmashauri

amewataka walimu wakuu kuanza mara moja zoezi la usajili wa wanafunzi wa mtihani wa mwaka 2027 sambamba na kuweka mipango madhubuti ya ufundishaji kwa wanafunzi

Na. Abdunuru Shafii

Afisa Elimu Awali na Msingi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma, Elestina Chanafi, amesema kutokana na mabadiliko ya mfumo wa elimu, kwa mara ya kwanza wanafunzi wa shule za msingi watahitimu wakiwa darasa la sita, hivyo maandalizi yanapaswa kuanza mapema ili kuhakikisha wanafunzi hao wanafanya vizuri katika mitihani yao.

Elestina ameyasema hayo wakati akiongoza kikao cha Elimu ngazi ya Halmashauri (DEM) cha Divisheni ya Elimu Awali na Msingi kilicholenga kufanya tathmini ya hali ya elimu pamoja na kuweka mikakati ya kuboresha ufaulu shuleni.

Kikao kilichoudhuriwa na Maafisa Elimu Kata kutoka kata 21 pamoja na walimu wakuu wa shule za msingi 89 za halmashauri hiyo.

Maafisa Elimu Kata na walimu wakuu wa shule za msingi halmashauri hiyo walioudhuria Kikao hicho.

Ambapo amewataka walimu wakuu kuanza mara moja zoezi la usajili wa wanafunzi wa mtihani wa mwaka 2027 sambamba na kuweka mipango madhubuti ya ufundishaji kwa wanafunzi watakaokuwa darasa la sita mwakani, ambao kwa sasa wapo darasa la tano.

Kwa upande wake, Afisa Elimu Vielelezo (Msingi) wa halmashauri hiyo, Respice Swetu, amesisitiza umuhimu wa kutatua changamoto zinazojirudia mashuleni kwa kuwataka walimu wakuu kuzisimamia ipasavyo, huku akiwakumbusha kuzingatia uadilifu kazini na kupambana na utoro.

Kwa upande wake, Afisa Elimu Vifaa na Takwimu (Msingi) wa halmashauri hiyo, Paul Joseph, amesema idara imepokea fedha za utekelezaji wa miradi mbalimbali ikiwemo ujenzi wa vyoo na nyumba za walimu, hivyo amewataka walimu wakuu kusimamia kwa karibu matumizi ya fedha hizo na kutoa ushirikiano unaohitajika.