Uvinza FM
Uvinza FM
15 April 2026, 8:20 pm

Kila mchezaji yuko focused kuelekea mchezo huu. Tunatambua utakuwa mgumu kwa sababu tunaiheshimu Singida Black Stars kama wapinzani wetu, lakini nasi tuna kikosi imara chenye wachezaji bora wazawa wenye uwezo wa kupambana na kupata matokeo chanya
Na. Abdunuru Shafii
Afisa Habari wa Mashujaa FC, Steven Ndorobo, amethibitisha kuwa kikosi cha timu hiyo kipo tayari kwa asilimia 100 kuelekea mchezo muhimu wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Singida Black Stars utakaopigwa kesho katika Uwanja wa Lake Tanganyika. Amesema wachezaji wote wako katika hali nzuri kimwili na kisaikolojia, wakiwa na morali ya juu ya kupambana kwa ushindi, huku habari njema ikiwa ni kurejea kwa nyota wao Mudhir Vuai na Jafary Kibaya waliokuwa majeruhi.
Hata hivyo, Ndorobo ameeleza kuwa Idris Istambuli ndiye mchezaji pekee atakayekosekana kutokana na majeraha ya muda mrefu, huku kikosi kingine chote kikiwa fiti na tayari kwa pambano hilo. Ameongeza kuwa maandalizi yamekamilika kwa kiwango cha juu na kila mchezaji anaelewa umuhimu wa mchezo huo katika mbio za ligi.
Katika hatua nyingine, uongozi wa timu hiyo umebainisha kuwa benchi la ufundi linaloongozwa na Julio Jamhuri Kihwelo limejipanga kuhakikisha linapata alama tatu muhimu. Wachezaji wamepewa mapumziko maalum ili kurejesha nguvu, huku mashabiki ‘Wanganyika’ na wadau wa soka Kigoma wakihimizwa kujitokeza kwa wingi uwanjani, wakiamini sapoti yao pamoja na rekodi nzuri ya nyumbani itakuwa chachu ya ushindi.
