Uvinza FM

Ukarabati MV liemba wafikia asilimia 75%

11 June 2026, 7:49 pm

Picha ya Katibu Tawala Mkoa wa Kigoma CPSP. Hassan Rugwa. picha na Abdunuru Shafii

mradi wa terminal ya kisasa ya abiria wenye thamani ya zaidi ya dola milioni 20 za Marekani unahusisha kuongeza kina cha bandari, kujaza maeneo maalum pamoja na ujenzi wa gati jipya lenye uwezo wa kuhudumia meli mbili kwa wakati mmoja. Mradi huo unatarajiwa kukamilika ifikapo Oktoba mwaka ujao.

Na. Abdunuru Shafii

Katibu Tawala wa Mkoa wa Kigoma, Hassan Rugwa, amesema miradi ya maboresho ya Bandari ya Kigoma katika Ziwa Tanganyika inaendelea vizuri na inatarajiwa kuongeza ufanisi wa huduma za usafiri wa majini na biashara ndani na nje ya nchi. Rugwa ametoa kauli hiyo baada ya kufanya ziara ya ukaguzi wa maendeleo ya ujenzi wa terminal mpya ya abiria pamoja na ukarabati wa meli ya MV Liemba.

Katika ziara hiyo, Rugwa pia alikagua maendeleo ya ukarabati wa meli ya kihistoria ya MV Liemba unaogharimu zaidi ya shilingi bilioni 26. Amesema ukarabati wa mradi huo umefikia zaidi ya asilimia 75 ya utekelezaji huku kazi zilizobaki zikiwa ni hatua za mwisho za ukamilishaji na majaribio ya meli.

Sauti ya Katibu Tawala Mkoa wa Kigoma CPSP. Hassan Rugwa. picha na Abdunuru Shafii

Kwa mujibu wa Rugwa, majaribio ya awali ya MV Liemba yanatarajiwa kuanza mwezi Julai kabla ya kuanza rasmi kutoa huduma mwezi Agosti. Meli hiyo ina uwezo wa kubeba abiria zaidi ya 600 na tani zaidi ya 200 za mizigo kwa safari moja, hali itakayoongeza fursa za usafirishaji na biashara katika ukanda wa Ziwa Tanganyika.

Amesema miradi hiyo ni sehemu ya juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan za kuimarisha usafiri wa majini nchini. Aidha, amewakaribisha wawekezaji na wafanyabiashara kutumia fursa zitakazotokana na maboresho hayo, huku akibainisha kuwa ukamilishaji wa MV Liemba utafungua njia ya kuanza kwa ukarabati wa meli nyingine ya kihistoria ya MV Mwongozo.

Sauti ya Katibu Tawala Mkoa wa Kigoma CPSP. Hassan Rugwa. picha na Abdunuru Shafii

Nae Humphrey Mwambungu kutoka Kampuni ya Meli Tanzania (TASHICO), amesema uwekezaji wa Serikali katika ukarabati wa meli ya Mv. Liemba utawanufaisha kiuchumi wananchi na wafanyabiashara wa ngazi zote kuanzia wajasiriamali hadi wafanyabishara wakubwa.

Aidha, Mwambungu amesema kuwa kwa sasa hakuna meli yenye uwezo wa kubeba watu na mizigo inayofanya kazi katika ziwa Tanganyika.

Sauti ya Humphrey Mwambungu kutoka Kampuni ya Meli Tanzania (TASHICO)