Uvinza FM
Uvinza FM
1 May 2026, 1:17 am

Katambi amewataka watanzania kutathmini athari za maisha ya ukimbizi jambo litakalowafanya waendelee kulinda amani ya nchi.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe. Patrobas Katambi amefunga rasmi Kambi ya wakimbizi ya Nduta iliyopo wilayani Kibondo mkoani hapa.
Kambi hiyo ilikuwa imehifadhi zaidi ya wakimbizi laki moja kutoka nchini Burundi ambao kwa sasa wamerejeswa kwenye nchi yao kufuatia hali ya amani na utulivu kutengemaa.
Kupitia Hotuba yake, Katambi amewataka watanzania kutathmini athari za maisha ya ukimbizi jambo litakalowafanya waendelee kulinda amani ya nchi.
Aidha, amesema Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na Burundi pamoja na Mashirika ya kimataifa, wamefanikiwa kuwarejesha jumla ya wakimbizi 165,494 kwa hali ya amani na utulivu.

Ameyashukuru mashirika yote yaliyokuwa yakitekeleza majukumu yao chini ya Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi (UNHCR), kwa mchango wao mkubwa tangu kuanzishwa kwa kambi hiyo mpaka kufungwa.
Pia ameushukuru uongozi wa mkoa pamoja na wakazi wa Wilaya ya Kibondo kwa kuridhia maeneo yao kutumika kwa ajili ya makazi ya wakimbizi sambamba na kukabiliana na changamoto mbalimbali zilizojitokeza kutokana na uwepo wa wakimbizi hao.
Kwa sasa Mkoa wa Kigoma umebakiwa na kambi moja ya wakimbizi ya Nyarugusu iliyopo Wilayani Kasulu ambapo serikali inaendelea na zoezi la urejeshaji ili iweze kufunga eneo la wakimbizi kutoka nchini Burundi.