Uvinza FM

Ni marufuku guta kusafirisha abiria

26 November 2026, 4:44 pm

wananchi wakiwa ndani ya Guta wakisikiliza maelezo ya Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Kigoma.

wananchi zingatieni sheria na kanuni za usalama barabarani kwa kutumia vyombo vya usafiri vinavyokidhi vigezo vya usalama.

Abdunuru Shafii

Jeshi la Polisi Mkoa wa Kigoma limewataka wananchi kuacha kutumia vyombo vya usafiri aina ya guta kubeba abiria, baada ya kubainika kwa baadhi ya wananchi kutumia vyombo hivyo kusafirisha watu wakiwemo watoto wadogo katika mazingira yanayoweza kuhatarisha usalama wao.

Wito huo umetolewa na Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Kigoma, Mrakibu Mwandamizi wa Polisi (SSP) Thimoth Chikoti, wakati akitoa elimu ya usalama barabarani kwa wananchi waliokuwa wakisafiri kwa kutumia guta eneo la Kitahana, Wilaya ya Kibondo.

wananchi wakiwa ndani ya Guta wakisikiliza maelezo ya Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Kigoma.

SSP Chikoti amesema kuwa vyombo hivyo havikutengenezwa kwa ajili ya kusafirisha abiria, hivyo matumizi yake kwa shughuli hizo yanaweza kuhatarisha maisha ya wanaovitumia, hususan watoto wadogo ambao wanahitaji uangalizi na ulinzi zaidi wanapokuwa safarini.

Aidha, amewasisitiza wananchi kuzingatia sheria na kanuni za usalama barabarani kwa kutumia vyombo vya usafiri vinavyokidhi vigezo vya usalama, akiwataka kutanguliza uhai wao na wa watoto wao badala ya kujiweka katika hatari zinazoweza kuepukika.