Uvinza FM
Uvinza FM
22 October 2026, 8:13 pm

Ushirikiano wa viongozi ni muhimu kuhakikisha wananchi wanapata matibabu wanapoyahitaji.
Na.Rehema Iddi
Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Balozi Simon Sirro, amewaagiza viongozi na watumishi wa umma kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za afya kupitia Mpango wa Bima ya Afya kwa Wote.
Ametoa agizo hilo wakati wa uzinduzi wa usajili wa Bima ya Afya kwa Wote Awamu ya Pili, uliofanyika katika Kituo cha Afya cha Rusimbi, mkoani Kigoma. Amesema ushirikiano wa viongozi ni muhimu kuhakikisha wananchi wanapata matibabu wanapoyahitaji.
Meneja wa Bima ya Afya Mkoa wa Kigoma, Gwamaka Mwakyoma, amesema katika awamu ya kwanza kaya 11,454 zilisajiliwa, sawa na asilimia 76.2 ya lengo la kaya 15,037. Kaya hizo zilikuwa na wanufaika 33,446 kati ya 65,755 waliolengwa.
Amesema awamu ya pili inalenga kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu umuhimu wa bima hiyo, usajili na namna ya kupata huduma za afya kupitia kadi zao.
Baadhi ya wananchi waliosajiliwa wameiomba Serikali kuboresha huduma za bima hiyo, wakisema ukosefu wa fedha unawafanya washindwe kupata matibabu, dawa na vipimo. Pia wameomba vifurushi viboreshwe ili viwezeshe upatikanaji wa huduma katika hospitali za rufaa na za kanda.