Uvinza FM
Uvinza FM
17 November 2026, 12:10 pm

Watuhumiwa hao tayari wamefikishwa mahakamani kwa hatua zaidi za kisheria
Na.Rehema Iddi
Jeshi la Polisi mkoani Kigoma limewakamata watuhumiwa watatu katika matukio mawili tofauti ya tuhuma za wizi, na kufanikiwa kuokoa mali zenye thamani ya mamilioni ya shilingi, ikiwemo mota ya maji na lita 160 za mafuta ya dizeli.
Akizungumza kuhusu matukio hayo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kigoma, Philemon Makungu, amesema tukio la kwanza lilitokea Oktoba 20, 2026, majira ya saa 3:10 asubuhi, katika eneo la Kibondo wilayani Kibondo, ambapo askari polisi waliokuwa doria waliwakamata watuhumiwa wawili wakiwa na mota moja ya maji inayodaiwa kuibwa katika chanzo cha maji wilayani humo.
Kamanda Makungu amesema mota hiyo yenye thamani ya shilingi milioni tisa inamilikiwa na Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Wilaya ya Kibondo. Ameongeza kuwa watuhumiwa hao tayari wamefikishwa mahakamani kwa hatua zaidi za kisheria.
Katika tukio jingine lililotokea Oktoba 27, 2026, katika Kijiji cha Mpeta wilayani Uvinza, askari polisi waliokuwa doria walimkamata mtuhumiwa mmoja akiwa na lita 160 za mafuta ya dizeli yanayodhaniwa kuwa mali ya wizi .
Amesema mtuhumiwa huyo atafikishwa mahakamani mara baada ya upelelezi wa tukio hilo kukamilika.