Uvinza FM

TAKUKURU yarejesha Sh Milioni 320 Kigoma

11 November 2026, 9:16 pm

Picha ya Kaimu Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Kigoma, John Mgallah, amesema Shilingi.Picha na Abdunuru Shafii

Miradi iliyoathirika ni ujenzi wa Soko la Kimataifa la Kagunga na jengo la Utawala la Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma Ujiji

Na.Rehema Iddi

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Kigoma imefanikiwa kurejesha Shilingi 320,904,775.35 zilizopotea kutokana na ubadhirifu na ukiukwaji wa taratibu za usimamizi wa fedha za umma, katika kipindi cha Aprili hadi Septemba 2026.

Akizungumza na waandishi wa habari, Kaimu Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Kigoma, John Mgallah, amesema Shilingi 260,178,775.35 zimerejeshwa katika Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma Ujiji na Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma, baada ya mkandarasi wa kampuni ya GOPA CONTRACTORS TANZANIA LIMITED kushindwa kutekeleza miradi na kutoweka na fedha za malipo ya awali.

Sauti ya Kaimu Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Kigoma, John Mgallah

Amesema miradi iliyoathirika ni ujenzi wa Soko la Kimataifa la Kagunga na jengo la Utawala la Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma Ujiji, huku fedha hizo zikirejeshwa baada ya juhudi za TAKUKURU kumtafuta na kumrejesha mkandarasi huyo mkoani Kigoma

Aidha, Mgallah amesema TAKUKURU imefanikiwa kurejesha Shilingi 230,000 kwa wananchi na Shilingi 60,496,000 Serikalini, akieleza kuwa hatua hiyo ni sehemu ya juhudi za kuhakikisha fedha za umma zinalindwa na kutumika kwa malengo yaliyokusudiwa.