Uvinza FM
Uvinza FM
10 November 2026, 3:15 pm

Wasimamizi kuimarisha uwazi na uwajibikaji kwa kuandaa taarifa za maendeleo ya miradi kila wiki na kuwashirikisha wataalamu pamoja na jamii.
Na.Rehema Iddi
Halmashauri ya Mji Kasulu imeendesha mafunzo maalumu kwa wasimamizi wa miradi ya maendeleo kutoka katika taasisi za umma, yakilenga kuimarisha usimamizi, uwajibikaji na matumizi sahihi ya fedha za miradi ili kuhakikisha inatekelezwa kwa wakati na kwa kuzingatia viwango vinavyotakiwa.
Mafunzo hayo yaliyotokana na maelekezo ya Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Mwl. Vumilia Julius Simbeye, yamewakutanisha Wakuu wa Shule, Walimu Wakuu na Waganga Wafawidhi. Akizungumza katika mafunzo hayo, Mkuu wa Kitengo cha Ufuatiliaji na Tathmini, Kyamani D. Kaijage, amesema Halmashauri inaendelea kutekeleza miradi mbalimbali ikiwemo ujenzi wa vyumba vya madarasa, ukarabati wa miundombinu na utengenezaji wa madawati, hivyo ni muhimu kwa wasimamizi kuhakikisha miradi hiyo inakamilika kwa wakati.
Kwa upande wake, Afisa Manunuzi na Ugavi, Onesmo Joseph, amesisitiza kuzingatiwa kwa sheria na taratibu za manunuzi ya umma pamoja na kushirikisha kamati husika, huku Mkaguzi wa Ndani, Tula Nkonko, akiwataka wasimamizi kuimarisha uwazi na uwajibikaji kwa kuandaa taarifa za maendeleo ya miradi kila wiki na kuwashirikisha wataalamu pamoja na jamii.
Washiriki wa mafunzo hayo pia wameeleza umuhimu wa makadirio ya gharama za miradi (BOQ) kuendana na fedha zilizotengwa na kuimarisha ushirikiano kati ya viongozi na wataalamu katika utekelezaji wake.
Mafunzo hayo yameandaliwa na Kitengo cha Ufuatiliaji na Tathmini kwa kushirikiana na Ofisi ya Manunuzi na Ugavi pamoja na Ofisi ya Mkaguzi wa Ndani.