Uvinza FM

Boti haramu 14 zataifishwa Uvinza na Gesti bubu yafungwa

21 November 2026, 11:09 pm

kama mnavyoona zimetengenezwa boti kubwa. Boti 14 tumezikamata kwa mujibu wa sheria zetu za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kuanzia sasa hizi boti 14 zote ni mali ya serikali na wote waliohusika
tutawakamata

Na. Abdunuru Shafii

Mkuu wa Wilaya ya Uvinza mkoani Kigoma, Mtela Mwampamba, ameagiza kutaifishwa kwa boti 14 za mizigo na uvuvi zenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 4.8 zilizokuwa zikitengenezwa kinyemela katika mwambao wa Ziwa Tanganyika, Kijiji cha Kabeba, Kata ya Mwakizega, huku akieleza kuwa eneo hilo limekuwa likiendesha shughuli zinazokiuka sheria na taratibu za nchi.

Akizungumza wakati wa ziara yake katika eneo hilo, Mwampamba amesema boti hizo zenye uwezo wa kubeba tani 200 kila moja zilikamatwa baada ya kubainika kuwa zinatengenezwa bila vibali halali, huku mbao na magogo yaliyotumika zikitokana na uharibifu wa mazao ya misitu yaliyohifadhiwa kisheria. Amesema kuanzia sasa boti zote 14 ni mali ya Serikali na wote waliohusika katika utengenezaji wake watachukuliwa hatua za kisheria.

Sauti ya Mkuu wa Wilaya ya Uvinza, Mtela Mwampamba kuhusu boti 14 kutaifishwa

Aidha, Mkuu huyo wa Wilaya amesema katika eneo hilo wamebaini uwepo wa gesti bubu iliyokuwa ikihifadhi mbao nyingi za miti aina ya mitipoli pamoja na mkaa, hivyo kuagiza kufungwa kwake mara moja na kutaifishwa kwa mazao hayo ya misitu. Ameongeza kuwa uchunguzi utafanyika pia kwa watumishi wa Serikali waliokuwa wakifanya kazi katika eneo hilo, akieleza kuwa licha ya uwepo wa viongozi na maafisa mbalimbali wa Serikali, uharibifu huo ulikuwa ukiendelea bila kuchukuliwa hatua.

Sauti ya Mkuu wa Wilaya ya Uvinza, Mtela Mwampamba, gesti bubu kufungwa

Mwampamba amesisitiza kuwa hatakubali mtu yeyote kutumia jina la viongozi wa juu wa Serikali kuhalalisha shughuli hizo, akieleza kuwa hakuna kibali wala maelekezo kutoka juu yaliyotolewa kuruhusu uharibifu huo, na kwamba kila mtumishi au mtu mwingine atakayebainika kuhusika atawajibishwa kwa mujibu wa sheria.

sauti ya Mkuu wa Wilaya ya Uvinza, Mtela Mwampamba, maelekezo kutoka juu