Uvinza FM

DED. Uvinza asisitiza nidhamu, uwajibikaji na weledi kazini

20 November 2026, 8:12 pm

Picha ya viongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Uvinza, na mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Uvinza, CPA Fred Milanzi akiwa amaongea na watumishi. Picha na winfrida Bwire

nidhamu ni msingi wa mafanikio katika utumishi wa umma, na mtumishi asiye na nidhamu hawezi kutoa huduma bora kwa jamii.

Na. Abdunuru Shafii

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Uvinza, CPA Fred Milanzi, amewataka watumishi wa Halmashauri hiyo kufanya kazi kwa nidhamu, uwajibikaji na weledi mkubwa ili kuhakikisha malengo yaliyokusudiwa yanatimia kwa wakati na ubora unaotakiwa.

CPA Milanzi ameyasema hayo leo Novemba 20, 2026, wakati akizungumza na watumishi wa Halmashauri katika kikao kilichofanyika kwenye ukumbi wa halmashauri ya Wilaya ya Uvinza Kama sehemu ya kujengeana uwezo na kukumbushana wajibu wa kazi.Amesema kuwa, nidhamu ni msingi wa mafanikio katika utumishi wa umma, na mtumishi asiye na nidhamu hawezi kutoa huduma bora kwa jamii.

Aidha, CPA Milanzi amesisitiza suala la uwajibikaji, ambapo kila mtumishi anatakiwa kuwajibika kwa kazi aliyokabidhiwa na kuhakikisha anatimiza malengo yaliyowekwa na Halmashauri. CPA Milanzi amewataka watumishi kuendelea kujifunza na kuboresha ujuzi wao ili waweze kwenda sambamba na mabadiliko ya teknolojia na mahitaji ya wananchi.

Picha ya baadihi ya watumishi. Picha na Winfrida

Kwa upande wake mkuu wa Wilaya ya Uvinza Mh.Mtela Mwampamba amehimiza Kila mfanyakazi kufanya kazi kwa kutumia taaluma yake ipasavyo ili kuleta mabadiliko chanya kwa jamii kama lilivyo lengo la serikali la kuwaletea wananchi maendeleo.

Naye Afisa Utumishi wa Halmashauri hiyo Ndg.Laurent Kapimpiti ametoa wito kwa watumishi hao kuvaa mavazi yenye hadhi ya kiutumishi na yenye kuleta heshima katika eneo la kazi.