Uvinza FM

Wananchi Kasulu wanufaika na kliniki ya Ardhi

7 November 2026, 10:33 pm

Picha ya baadhi ya wananchi wa kasulu waliopokea hati miliki ya ardhi.Picha na Rehema Iddi

Huduma za Ardhi kliniki zilizotolewa na Ofisi ya Kamishna wa Ardhi Mkoa wa Kigoma

Na.Abdunuru  Shafii

Wananchi wa Kijiji cha Nyangwa, Kata ya Makere Wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma, wamepatiwa hati miliki za viwanja vyao kupitia huduma za Ardhi kliniki zilizotolewa na Ofisi ya Kamishna wa Ardhi Mkoa wa Kigoma, hatua inayolenga kusogeza huduma za ardhi karibu na wananchi na kupunguza changamoto za gharama za usafiri kufuata huduma hizo mjini Kigoma.

Akizungumza wakati wa zoezi hilo, Kamishna wa Ardhi Mkoa wa Kigoma, Yustha Byabusha amesema eneo hilo lilipangwa na kupimwa mwaka 2022 ambapo jumla ya viwanja takribani 800 vilipimwa, huku hadi sasa hati miliki 385 zikiwa zimetolewa kwa wananchi. Amesema hatua ya kupeleka huduma hizo kijijini imetokana na umbali wa zaidi ya kilomita 100 kutoka eneo hilo hadi ofisi za ardhi mkoani Kigoma, pamoja na lengo la kuwapatia wananchi fursa ya kupata hati miliki, kutatua migogoro ya ardhi na kutoa elimu kuhusu mfumo mpya wa utoaji huduma za ardhi

Sauti ya Kamishna wa Ardhi Mkoa wa Kigoma, Yustha Byabusha

Kwa upande wake, Katibu wa Urasimishaji Ardhi wa Kata ya Makere, Vincent Stefano Ruhinya, ameishukuru Ofisi ya Kamishna wa Ardhi kwa kufikisha huduma hizo katika eneo hilo, akisema amekuwa akishirikiana na wataalamu katika zoezi la upimaji wa maeneo ya wananchi na kwamba kuletwa kwa huduma hizo kumewawezesha wananchi kupata hati miliki bila kulazimika kusafiri umbali mrefu.

Sauti ya Katibu wa Urasimishaji Ardhi wa Kata ya Makere, Vincent Stefano Ruhinya

Nao Baadhi ya wananchi waliofaidika na zoezi hilo wameeleza kufurahishwa na upatikanaji wa hati miliki katika maeneo yao, wakisema hapo awali walikabiliwa na changamoto za nauli na gharama za kufika mjini Kigoma, huku wengine wakishindwa kufuatilia hati hizo kutokana na kukosa sehemu za kufikia wanapokuwa mjini. Wameishukuru Serikali kwa kusogeza huduma hizo karibu, wakieleza kuwa hati miliki zitawasaidia kuwa na uhakika wa kisheria wa umiliki wa maeneo yao.

Sauti ya baadhi ya wananchi walio pokea hati miliki