Uvinza FM
Uvinza FM
26 October 2026, 11:09 am

Kigoma tayari imeunganishwa na gridi ya taifa na kupokea megawati 54, hivyo kuondoa changamoto ya kutegemea majenereta.
Na. Rehema Iddi
Katibu Tawala wa Mkoa wa Kigoma, Hassan Rugwa, amesema kuimarika kwa upatikanaji wa umeme mkoani humo kutafungua fursa zaidi za uwekezaji katika sekta ya viwanda na kukuza uchumi wa mkoa.
Akizungumza wakati wa kukagua ujenzi wa Kituo cha Kuzalisha Umeme cha Malagarasi, kinachotarajiwa kuzalisha megawati 49.5, Rugwa amesema Kigoma tayari imeunganishwa na gridi ya taifa na kupokea megawati 54, hivyo kuondoa changamoto ya kutegemea majenereta.
Rugwa amemtaka mkandarasi kuongeza kasi ya ujenzi wa mradi huo unaoendelea nyuma ya muda uliopangwa, huku akisisitiza kuchukua tahadhari dhidi ya athari zinazoweza kusababishwa na mvua kubwa.
Kwa upande wake, Kaimu Mratibu wa Mradi kutoka TANESCO, Mhandisi Majubwa Mzungu, amesema mradi umefikia asilimia 31.7, huku kazi zinazoendelea zikihusisha ujenzi wa tuta kuu, njia za maji na misingi ya mitambo ya kuzalisha umeme.
Mradi huo wenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 300 unatarajiwa kukamilika Oktoba 2027. Ukikamilika, utaongeza uzalishaji wa umeme katika gridi ya taifa na kusaidia kupunguza changamoto ya upatikanaji wa umeme mkoani Kigoma.