Mufindi FM
Mufindi FM
3 November 2026, 10:55 am

Wazazi na walezi wametakiwa kuchagua shule salama na zinazotambuliwa na serikali ili kuhakikisha watoto wanapata elimu na malezi bora katika mazingira salama.
Na Jackson Machowa
Wazazi, walezi na jamii wametakiwa kuwa makini katika kuchagua shule na vituo vya kulelea watoto kwa kuhakikisha vinatambulika na kuthibitishwa na mamlaka za serikali ili kulinda usalama wa watoto na kuhakikisha wanapata malezi bora pamoja na elimu katika mazingira salama.
Wito huo umetolewa na Afisa Maendeleo ya Jamii wa Halmashauri ya Mji wa Mafinga mkoani Iringa, Bi. Leah Charles, wakati akizungumza na wazazi, walezi na wananchi waliohudhuria mahafali ya nne ya darasa la awali katika Shule ya Awali na Msingi ya The Bright, iliyopo Mtaa wa Ndolezi mjini Mafinga.
Bi. Charles amesema kumekuwa na ongezeko la matukio ya ukatili na mmomonyoko wa maadili kwa watoto, hususan wa kiume, akibainisha kuwa baadhi ya matukio hayo yanachangiwa na mapungufu katika malezi yanayotolewa na baadhi ya wazazi, walezi na walimu, hali inayohatarisha usalama na ustawi wa watoto katika jamii.

Kwa upande wake, Mkuu wa Shule hiyo, Mwalimu Jonathan Besisila, amesema Shule ya The Bright Day Care Pre and Primary imejikita katika kuhakikisha watoto wanapata malezi na makuzi bora yanayozingatia taaluma na maadili, kwa kusimamia ipasavyo maendeleo yao ili kuwawezesha kutimiza ndoto zao.
Naye Mkurugenzi wa shule hiyo, Mwalimu Luca Mang’uli, amewasihi wazazi na walezi wa watoto waliohitimu elimu ya awali kuhakikisha wanaendelea na elimu ya msingi katika shule hiyo ili kuendeleza misingi ya taaluma na malezi waliyoipata.
Mgeni rasmi katika mahafali ya nne ya darasa la awali ya Shule ya The Bright Day Care Pre and Primary, Mwalimu Sambala Kastory, ambaye ni Afisa Elimu Taaluma wa Halmashauri ya Mji wa Mafinga, amewataka wazazi na walezi kujiandaa mapema kwa ajili ya masomo ya watoto wao kuelekea mwaka mpya wa masomo Januari 2027, huku akiitaka jamii kushiriki kikamilifu katika ukuaji na maendeleo ya shule hiyo kutokana na mchango wake katika utoaji wa elimu na malezi bora kwa watoto…
