Mufindi FM

Vituo 56 vya huduma kwa wakulima vyapatiwa msukumo mpya na WFP

13 October 2026, 2:08 pm

Wahitimu wa vituo 56 vya kutoa huduma kwa wakulima nyanda za juu kusini wakiwa katika shehere ya kuhitimu baada ya kuwezeshwa kwa miaka minne na mradi wa FtMA unaofadhiliwa na WFP. Picha na Kelvin Ayubu

Hatua ya kuhitimu kwa watoa huduma wa vituo vinavyohudumia wakulima kunatajwa kuwa chachu ya mafaniko katika sekta ya kilimo kwa kurahisisha upatikanaji wa elimu na matumizi ya dhana bora kwa wakulima.

Na Jackson Machowa

Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) limekabidhi vifaa vyenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 50 kwa baadhi ya vituo vya kuhudumia wakulima katika mikoa ya Iringa, Njombe na Mbeya, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuimarisha huduma za kilimo na kuongeza uzalishaji wa mazao yenye tija sokoni.

WFP ambayo ni mwezeshaji wa mradi wa Farm to Market Allience(FtMA)unaotekelezwa na shirika la Nafaka Kilimo imekabidhi vifaa hivyo wakati wa sherehe ya kuhitimu kwa vituo 56 vya kutoa huduma kwa wakulima zilizofanyika manispaa ya Iringa mkoani humo.

Akizungumza katika hafla hiyo, mwakilishi wa Mkurugenzi Mkazi wa WFP ambaye pia ni Mkuu wa Kitengo cha Ugavi wa shirika hilo jijini Dodoma, Mahamood Mabuyu, amesema uwekezaji huo ni sehemu ya juhudi za shirika hilo za kutokomeza njaa na kuimarisha usalama wa chakula na lishe duniani.

Sauti ya mwakilimishi wa mkurugenzi mkazi wa WFP na mkuu wa kitengo cha ugavi Mahamood Mabuyu

 Kwa upande wake mratibu wa mradi wa FtMA Nyanda za juu kusini Bwana Mosses Logan amesema waliohitimu ni wanufaika wa mradi walioandaliwa kuwa kiunganishi kati ya wakulima na wadau wengine katika mnyororo wa thamani wa kilimo huku mkurugenzi mkuu wa mradi huo kutoka nchini Kenya Anastasia Mbatia akitoa rai kwa wahitimu kuendelea kuwahudumia wananchi.

Sauti ya mratibu wa mradi wa FtMA Mosses Logan wakwanza kuzungumza pamoja na Anastasia Mbatia ambaye ni mkurugenzi mkuu wa FtMA wapili kuzungumza

Wakati huohuo, mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo anayeshughulikia masoko na usalama wa chakula, Patrick Mongela, amesema Serikali inathamini mchango wa washirika wa maendeleo katika kuendeleza sekta ya kilimo na kufanikisha utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2050.

Sauti ya mwakilishi wa katibu mkuu wizara ya kilimo anayeshughulikia masoko na usalama wa chakula Patrick Mongela
Picha ya baadhi ya vifaa vilivyokabidhiwa kwa wahitimu wa vituo vya kutoa huduma kwa wakulima

Vifaa vilivyokabidhiwa  ni Mizani, Turubai na vipima unyevu ambavyo vitatumiwa na watoa huduma waliohitimu kutoka wilaya za Iringa,Mufindi na Kilolo mkoani Iringa, Wanging’ombe mkoani Njombe na Mbarali mkoani Mbeya.