Mufindi FM

Watumishi Mufindi DC wapigwa msasa uwekezaji dhamana BoT

14 April 2026, 11:16

Watumishi wa halmashauri ya wilaya ya Mufindi wakipewa elimu kuhusu namna ya kushiriki katika soko la awali na la pili la uwekezaji wa dhamana za serikali za muda mrefu na mfupi, yaliyoratibiwa na Benki kuu ya Tanzania (BoT) Kanda ya Mbeya yaliyofanyika katika ofisi za bomani zilizopo katika mji wa Mafinga wilaya hapo. Picha na Marko Msafiri.

Uwekezaji huu ni salama na una tija kubwa sana kwa muwekezaji

Na Marko Msafiri

Benki Kuu ya Tanzania (BoT) tawi la Mbeya imeendesha semina ya mafunzo kwa watumishi wa Halmashauri ya wilaya ya Mufindi, mkoani Iringa, yakilenga kuwezesha uelewa na kushiriki kikamilifu kwenye uwekezaji wa dhamana za serikali kwa usahihi na ufanisi.

Mafunzo hayo yamefanyika katika ukumbi wa Bomani uliopo Mafinga, yakihusisha watumishi mbalimbali wa umma kutoka halmashauri hiyo kuhusu namna ya kushiriki katika soko la awali na la pili la dhamana za serikali za muda mrefu na mfupi.

Akizungumza baada ya mafunzo hayo, Meneja fedha na utawala wa BoT Tawi la Mbeya, Bi. Marrystela Kamuzola, amesema kuwa uwekezaji katika dhamana za serikali ni salama na una faida kwa wawekezaji.

Sauti Bi. Kamuzola faida uwekezaji.

Aidha Bi. Kamuzola ameweka wazi kuhusu dhamana na aina zake, akieleza kuwa dhamana hizo zimegewanyika katika makundi mawili,yaani dhamana za muda hrefu na za muda mfupi ambapo mwekezaji hupata faida kulingana na muda wa aina ya uwekezaji wake.

Sauti Bi Kamuzola

Pia Bi. Kamuzola ameongeza kuwa, kupitia uwekezaji huo, watumishi wa umma wanaweza kupanga vizuri matumizi ya kipato chao, kuweka akiba na kujiwekea msingi imara wa kifedha kwa muda mrefu.

Pichani ni Meneja fedha na utawala wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) Tawi la Mbeya, Bi. Marrystela Kamuzola akitoa elimu ya uwekezaji kwa watumishi hao. Picha na Marko Msafiri.

Awali akizungumza mgeni rasmi wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo, mkuu wa wilaya ya Mufindi Dkt. Linda Salekwa amewahimiza watumishi wa umma kuwekeza katika dhamana hizo za serikali ili kujenga usalama wa kifedha na kujiepusha na mikopo yenye riba kubwa maarufu kama kausha damu.

Dkt. Salekwa amesema watumishi wengi watumishi wengi wamekuwa wakiingia katika mikopo isiyo rafiki kutokana na ukosefu wa elimu sahihi ya uwekezaji, hali inayoweza kuathiri ustawi wao wa kifedha.

Nao baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo, akiwemo afisa mtendaji wa kijiji cha Lugolofu kata ya Makungu, Lucy Kiwela wameeleza kuwa elimu hiyo, imewapa mwanga mpya kuhusu uwekezaji salama, wakiahidi kuitumia kuboresha hali zao za kifedha.

Sauti washiriki

BoT inaendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu dhamana za serikali ikiwa ni sehemu ya juhudi za kukuza uelewa wa masoko ya fedha na kuongeza ushiriki wa wananchi katika uwekezaji.