Mufindi FM

Zaidi ya majiko 1700 ya nishati safi yauzwa kwa ruzuku mufindi

14 May 2026, 10:43 am

Pichani ni Mkuu wa wilaya ya Mufindi Mhe. Dkt. Linda Salekwa, Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya wilaya hiyo Ndg. Mashaka Mfaume na Mkurugenzi mtendaji wa kampuni ya Green Way Bi. Sabitina Makweta wakati wa uzinduzi wa mnada wa uuzaji wa majiko banifu ya kuni na mkaa katika makao makuu ya halmashauri hiyo Itulavanu. Picha na Kelvin Ayoub.

Kwa mujibu wa tafiti zilizofanywa zinaonyesha kuwa matumizi ya nishati chafu ya kupikia hasa kuni na mkaa kwa siku moja ni sawa na kuvuta sigara 300.

Na Kelvin Ayoub

Serikali imeendelea na jitihada za kuhakikisha wananchi wanatumia nishati safi na salama baada ya majiko 1736 ya nishati safi ya mkaa na kuni kuuzwa kwa bei ya ruzuku katika Wilaya ya Mufindi, mkoani Iringa.

Akizungumza Wakati akizindua mnada wa hadhara wa uuzaji wa majiko uliofanyika katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi, makao makuu ya Itulavanu, Mkuu wa Wilaya ya Mufindi Dkt. Linda Salekwa amesema hatua hiyo ni sehemu ya mikakati ya serikali ya kurahisisha upatikanaji wa nishati safi kwa wananchi pamoja na watumishi wa umma.

Dkt. Salekwa ameongeza kuwa matumizi ya nishati safi yatasaidia kupunguza athari za kiafya zinazotokana na matumizi ya nishati zisizo salama, huku akiwasihi wananchi kujitokeza kwa wingi kutumia fursa hiyo muhimu.

Sauti Dkt. Linda Salekwa

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi Ndg. Mashaka Mfaume amesema serikali imeamua kutoa ruzuku kubwa kwa majiko hayo ili kuhakikisha hata wananchi wa kipato cha chini wanamudu kuyapata kwa urahisi.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Green Way Bi Sabitina Makweta amesema jumla ya majiko 5726 yameuzwa kwa bei ya ruzuku katika Mkoa wa Iringa, ambapo majiko 1736 yamesambazwa ndani ya Wilaya ya Mufindi pekee ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa sera ya taifa ya matumizi ya nishati safi.

Sauti Mkurugenzi Green Way

Ameeleza kuwa jiko ambalo bei yake halisi ni shilingi elfu sabini na mbili na mia tano, sasa linauzwa kwa shilingi elfu kumi na mbili na mia mbili pekee, huku serikali ikigharamia zaidi ya asilimia 80 ya gharama hizo.

Kwa upande wao, wananchi waliojitokeza katika mnada huo wameishukuru serikali pamoja na wadau mbalimbali wakiwemo Wakala wa Nishati vijijini (REA) kampuni ya Green Way na Ecomama kwa kuwezesha upatikanaji wa majiko hayo kwa bei nafuu.

Sauti Wananchi

Wananchi kutoka maeneo mbalimbali ndani ya halmashauri ya wilaya hiyo wakiwa wamejitokeza katika uzinduzi wa mnada huo ikiwa ni jitihada zinazofanywa na serikali za kuwaondolea wananchi athari za kiafya ikiwemo magojwa katika mfumo wa upumuaji yanayochochewa na matumizi hayo ya nishati chafu. Picha na Kelvin Ayoub.

Mnada huo wa hadhara umefanyika katika ukumbi wa Halmashauri ya Mufindi Itulavanu, huku wananchi wengi wakijitokeza kununua majiko hayo rafiki kwa mazingira na afya.