Mufindi FM

Vitabu 4,559 vya sayansi kusambazwa wilayani Malinyi

26 September 2023, 10:29

Wakuu wa shule za sekondari wilayani Malinyi katika picha ya pamoja baada ya kukabidhiwa vitabu na kaimu mkurugenzi mtendaji wilaya bwana Gasto Silayo kwenye hafula iliyofanyika katika viwanja vya shule ya msingi nawigo. Picha na Jackson Machoa.

Vitabu hivyo vitasaidia kuchochea ufaulu wa wanafunzi kwa masomo ya sayansi.

Na Jackson Machoa – Morogoro

Jumla ya vitabu 4559 vya masomo ya sayansi vimekabidhiwa na kusambazwa katika shule mbalimbali za sekondari wilayani Malinyi mkoani Morogoro ili kukabiliana na changamoto ya uhaba wa vitabu hivyo mashuleni.
Akizungumza katika hafla ya ugawaji wa vitabu hivyo kwa wakuu wa shule mbalimbali wilayani humo iliyofanyika katika viwanja vya shule ya msingi Nawigo, kaimu mkurugenzi mtendaji wilaya Bw. Gasto Silayo ameishukuru serikali kwa kazi kubwa inayofanyika na kuwataka walimu kuhakikisha vitabu hivyo vinawafikia wanafunzi na kutumika ipasavyo.

Sauti ya Kaimu DED Malinyi

Aidha Bw. Silayo ameongeza kuwa halmashauri inayo mipango na mikakati mbalimbali yenye lengo la kuwezesha upatikanaji wa miundombinu rafiki kwa walimu na wanafunzi ili kuweza kuinua kiwango cha taaluma wilayani humo.
Kwa upande wake mkuu wa divisheni ya elimu sekondari wilayani humo bi Pendo Masalu amewataka walimu kuwahimiza wanafunzi kusoma na kuvitunza vitabu hivyo ili viweze kutumika kwa muda mrefu na kuwasaidia wanafunzi wengi zaidi.

Sauti ya Bi Pendo
Vitabu hivyo 4,559 vyenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni ishirini na laki saba vinawahusisha wanafunzi wa kidato cha kwanza hadi cha nne kwa masomo ya hisabati na biolojia.