Mufindi FM

“Umoja Songea Mafinga Mjini” wafanya matendo ya huruma watoto wenye uhitaji

11 May 2026, 7:36 pm

Pichani ni umoja wa wakazi wanaoishi katika mji wa Mafinga kutoka Songea mkoani Ruvuma, watoto wanaolelewa katika kituo cha Yerusalem kilichopo mjini hapo sambamba na mlezi wa watoto hao Sister. Dativa Msilu, baada ya kukabidhi mahitaji mbalimbali ya watoto hao kituoni hapo. Picha na Kelvin Ayoub .

Na Kelvin Ayoub

Umoja wa Wakazi wa Songea mkoani Ruvuma, wanaoishi katika mji wa Mafinga wametembelea kituo cha watoto wenye uhitaji maalumu cha Yerusalem pamoja na shule ya msingi mchanganyiko Makalala, na kutoa msaada wa mahitaji mbalimbali ikiwa ni sehemu ya kuonesha upendo kwa watoto hao.

Miongoni mwa mahitaji yaliyotolewa ni pamoja na mchele kilo 50, mafuta ya kupikia, vinywaji pamoja na nguo kwa ajili ya watoto hao, huku tukio hilo likigusa mioyo ya wengi waliohudhuria.

Akizungumza wakati wa kukabidhi msaada huo, Mwenyekiti wa umoja huo, Bw. Paulo Nyoni amesema dhamira yao ni kuendelea kuwafikia na kuwasaidia wenye uhitaji kila inapowezekana, akieleza kuwa kufanya hivyo ni sehemu ya sadaka na moyo wa upendo kwa jamii.

Sauti Mwenyekiti wa umoja huo.

Aidha, viongozi na wanachama wa umoja huo wameeleza furaha yao baada ya kushiriki katika tukio hilo, huku wakitoa wito kwa jamii kuendelea kufanya matendo ya huruma na kusaidia watoto wenye uhitaji maalumu katika vituo mbalimbali.

Sauti wanachama wa umoja huo

Kwa upande wao, watoto pamoja na viongozi wa vituo hivyo wameushukuru uongozi wa kikundi hicho kwa kuwapatia msaada na kuwafanya kuwa sehemu ya jamii, wakieleza kuwa hatua hiyo imewapa faraja, matumaini na hisia za kuthaminiwa.

Sauti viongozi na watoto

Umoja huo umeendelea kuwa mfano mzuri katika jamii kwa kujenga mshikamano, kusaidiana na kushiriki shughuli za kijamii zinazolenga kugusa maisha ya watu wenye uhitaji.

Wanachama wa umoja huo na baadhi ya watoto wenye uhitaji katika kituo cha Jerusalem kilichopo katika mji wa Mafinga wakifanya maombi katika kituo hicho. Picha na Kelvin Ayoub.

Matendo hayo ya huruma yameendelea kuonyesha kuwa mshikamano na upendo vinaweza kuwa chachu ya matumaini na faraja kwa makundi yenye uhitaji maalumu katika jamii.