Mufindi FM
Mufindi FM
6 June 2025, 1:46 pm

Katika picha ni Madaktari bingwa wa kinywa na meno wakimufanyia matibabu mgonjwa wa meno katika kituo cha afya Usokami. Picha na Marko Msafiri.
Kabla ya ujio wa Madaktari Bingwa katika kituo hicho, wananchi walilazimika kusafiri umbali mrefu hadi hospitali kubwa huduma za kibingwa hali iliyosababisha gharama kubwa, usumbufu na kuchelewa kupata matibabu.
Na Marko Msafiri
Wananchi wa Kata ya Ihalimba, Kibengu, Mapanda na maeneo jirani wamepata fursa ya kipekee ya huduma za matibabu ya kibingwa na kibobezi yanayofanyika katika kituo cha afya cha Usokami baada ya uzinduzi rasmi wa kambi ya madaktari bingwa kutoka Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) na Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Iringa.
Kambi hiyo imelenga kutoa huduma za uchunguzi na matibabu katika maeneo mbalimbali ya afya ikiwa ni pamoja na matibabu ya kinywa na meno, Watoto, wakinamama na wajawazito, Daktari bingwa wa upasuaji wa jumla (general surgery), magonjwa ya ndani.
Akizungumza mara baada ya uzinduzi, Mratibu wa kambi hiyo Prof. Obadia Venance Nyongole ambaye kitaaluma ni Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Sayansi na Afya Shirikishi Muhimbili, amesema uwepo wa kambi hiyo katika kituo hicho ni kufuatia hapo awali kupokea maombi ya kuhitaji kusogeza huduma bora kwa wananchi, lengo ikiwa ni kuunga juhudi zinazofanywa na serikali katika kutoa huduma kwa wananchi hata waliopo katika maeneo ya pembezoni.
Sauti Prof. Nyongole
Kwa upande wake, Mganga Mfawidhi wa Kituo hicho Dkt. Ambonisye Mpangule amewasihi wananchi kutumia fursa ya uwepo wa madaktari hao bingwa katika kutatua changamoto zao za kiafya sambamba na kupunguza gharama ikiwemo hapo awali kusafiri umbali mrefu kufuata huduma hizo.
Sauti Mganga Mfawidhi
Nao wananchi ambao ni wanufaika wa huduma hizo akiwemo Frola Lugangala mkazi wa Winome iliyopo katika Halmashauri ya Kilolo mkoani Iringa wamepongeza hatua hiyo na kuiomba serikali iendelee kuwezesha mpango huo.
Kituo cha afya cha Usokami ni taasisi binafsi inayomilikiwa na parokia ya Usokami Jimbo Katoliki la Mafinga.