Mufindi FM
Mufindi FM
17 June 2026, 8:32 pm

Diwani wa kata ya Mdabulo Mhe. Marko Shayo akizungumza na wananchi wa kijiji cha Ihefu kilichopo katika kata hiyo, wakati wa mkutano wa hadhara uliohusisha usikilizaji wa kero mbalimbali. Picha na Marko Msafiri.
Kwa mujibu wa taarifa ni kwamba, vijana wengi wa kijiji hicho wanategemea mali za urithi kutoka kwa wazazi wao jambo linalowafanya kubweteka na kushindwa kujishughulisha na shughuli halali za kujiingiza kipato.
Na Marko Msafiri
Vijana saba kutoka kijiji cha Ihefu, kata ya Mdabulo, wamepoteza maisha kati ya mwaka 2010- 2026 kutokana na kuhusishwa na matukio ya wizi katika maeneo mbalimbali nje ya kijiji, takwimu ambazo zimeelezwa kuwa ni ishara ya hatari kubwa inayotokana na changamoto ya malezi kwa watoto na vijana.
Kutokana na hali hiyo, wazazi na walezi katika kijiji hicho, wamehimizwa kuongeza juhudi katika malezi na makuzi ya watoto wao ili kuwakinga dhidi ya vitendo vya uhalifu vinavyoweza kuhatarisha maisha yao na usalama wao.
Akizungumza wakati wa Mkutano wa Hadhara uliofanyika katika kijiji hicho, Mwenyekiti wa kijiji. Mhe. Chesco Mhwagila amesema takwimu zinatisha na zinaonesha umuhimu wa jamii kuchukua hatua za pamoja katika kuwalea na kuwalekeza vijana kwenye maadili mema na shughuli halali za kujipatia kipato.
Sauti Mwenyekiti Mhwagila

Pichani ni Mhe. Marko Shayo ambaye ni Diwani wa kata ya Mdabulo akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Ihefu kilichopo katika kata hiyo katika mkutano wa hadhara alioufanya hivi karibuni. Picha na Marko Msafiri.
Kwa upande wake, Inspekta Hoseah Mwakiluma ambaye ni Polisi Jamii wa Kata ya Mdabulo, amesikitishwa juu ya ongezeko la vitendo vya uhalifu vinavyofanywa na baadhi ya vijana wanaodaiwa kuwa wahalifu, akivitaja vitendo vya ujambazi wa kutumia silaha na unyanganyi.
Sauti Inspekta. Hoseah Mwakilima
Naye Diwani wa kata hiyo ya Mdabulo, Mhe. Marko Shayo amewataka wazazi kuwakemea na kuwaonya vijana wao, pale wanaposikia tetesi zao za kujiingiza katika matendo hayo ya uhalifu kwani mwisho wa vitendo hivyo huwa ni mbaya.
Sauti Mhe. Diwani

Diwani wa kata ya Mdabulo Mhe. Marko Shayo akisisitiza juu ya wajibu wa wazazi malezi katika malezi ya watoto na vijana ili kuwajengea misingi mema ya maadili katika jamii. Picha na Marko Msafiri.
Ponziano Kigahe ambaye ni Afisa Mtendaji wa Kijiji hicho, amewapongeza vijana wanaofanya kazi halali, huku akilaani matukio hayo ya vitendo vya uhalifu katika kijiji hicho.
Sauti mtendaji kijiji
Hali kadhalika, Mkurugenzi wa shirika la kujiletea maendeleo Vijijini (RDO). Ndg. Fidelis Emilio Filipatali amewataka wananchi wa kijiji hicho, kutumia vyuo vya ufundi vya shirika hilo, ili kupata ujuzi utakaowawezesha kunufaika na mikopo ya ujasiriamali inayotolewa na halmashauri jambo litakalowafanya vijana kujikita zaidi na kazi halali na si vitendo hivyo viovu.

Sauti Mkurugenzi RDO
Mkurugenzi wa shirika la kujiletea maendeleo Vijijini (RDO) ndugu. Fidelis Emilio Filipatali akizungumza na wananchi wa Kijiji hicho cha Ihefu, kuhusu kutumia vyuo vya shirika hilo ili kupata ujuzi utakaowawezesha kunufaika na mikopo ya wajasiriamali inayotolewa na halmashauri. Picha na Marko Msafiri.