Mufindi FM

Mbunge Villa agawa meza za biashara, wajasiriamali 160 kunufaika

14 April 2026, 18:30

Mbunge wa jimbo la Mafinga Mjini Mhe. Dickson Nathan Lutevele (Villa) akiwa na miongoni mwa wanufaika wa meza hizo za biashara wakiwa katika soko la Mashujaa lililopo katika mji huo, ikiwa ni jitihada za kuwatengenezea mazingira wezeshi ya ufanyaji wa biashara. Picha na Marko Msafiri.

Naomba nianze na hawa wachache, ili kuwapunguzia safari ya kutembea mtaani kutwa nzima ili nao waweze kusomesha watoto kupitia biashara wanayoifanya- Villa.

Na Jackson Machowa

Mbunge wa Jimbo la Mafinga Mjini Wilayani Mufindi Mh.Dickson Lutevele (Villa) amekabidhi meza za biashara kwa wajasiriamali 95 wa masoko mbalimbali mjini Mafinga kama sehemu ya kuboresha mazingira ya biashara na kuinua uchumi wa wananchi.

Mhe. Lutevele amekabidhi meza hizo mbele ya mamia ya wafanyabiashara, wajasiriamali na wananchi waliojitokeza katika hafla iliyofanyika kwenye viwanja vya soko la Mashujaa ikiwa ni awamu ya kwanza ya ugawaji wa meza hizo huku awamu ya pili ikitarajiwa kuwanufaisha wajasiliamali 65 na kufanya jumla wanufaika kufikia 160.

Akizngumza na umati uliojitokeza kumsikiliza Mh. Lutevele amesema katika kipindi cha miaka mitano ya uongozi wake atajitahidi kugusa maisha ya kila mwananchi kwa kadri itakavyowezekana huku akiwasihi wajasiliamali kuachana na mikopo umiza na kuchangamkia mikopo ya halmashauri yenye mazingira wezeshi ya kumkomboa mwananchi.

Sauti Mbunge Mhe Villa

Katika hafla hiyo ambayo iligeuka kikao kazi kilicholenga kusikiliza na kutatua kero za wananchi, Mhe. Lutevele amesisitiza kuendelea kuzishughulikia changamoto kubwa za miundombinu ya barabara na maji ili kuendelea kuchochea na kurahisisha shughuli za ukuaji wa uchumi na maendeleo ya watu.

Sauti wananchi & Mhe. Villa

Mbunge wa Jimbo la Mafinga Mjini Mhe. Dickson Nathan Lutevele (Villa) akizungumza na wananchi wa jimbo hilo. Picha na Marko Msafiri.

Kwa upande wao baadhi ya wajasiriamali walionufaika na awamu ya kwanza wa mgao wa meza hizo za biashara akiwemo bi Enea Malenda na Winfrida Kikoti wamesema meza hizo zitaongeza thamani ya bidhaa zao na kuwapumzisha dhidi ya safari ndefu za matembezi ya mauzo mitaani.

Wananchi wa jimbo la Mafinga Mjini wakiwa katika mkutano wa Mbunge wa Jimbo hilo Mhe. Dickson Nathan Lutevele (Villa) ulioambatana na ugawaji wa meza za biashara kwa wajasiriamali na usikilizwaji wa kero zinazowakumba. Picha na Marko Msafiri.