Mufindi FM

TFS yaongeza nguvu kupambana na moto, zaidi ya 400 wahojiwa Sao Hill

24 June 2026, 2:21 pm

Msaidizi wa Mhifadhi mkuu wa shamba la miti la Sao hill ambaye pia ni Msimamizi wa kitengo cha uendelezaji rasilimali Misitu na Nyuki, Ndgu. PCO Said Singano akizungumza na baadhi ya vijana waliojitokeza kwenye usaili, uliofanyika katika viwanja vilivyopo makao makuu ya wakala huo, kwa ajili ya kuomba kujiunga na vikosi vya kupambana na janga la moto, ikiwa ni maandalizi kuelekea kipindi cha kiangazi.

Takwimu zinaonesha kuwa matukio ya moto yamekuwa yakisababisha uharibifu mkubwa wa misitu katika Shamba la Miti la Sao hill, ambapo kwa mwaka 2024, hekta 400 za mashamba ya serikali pamoja na hekta 200 za wananchi binafsi ziliteketea katika moto ulioripotiwa eneo la Wami.

Na Kelvin Ayoub

Wakala la Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kupitia Shamba la Miti la Sao hill wilayani Mufindi umeendesha zoezi la usaili kwa vijana zaidi ya 400 walioomba kujiunga na vikosi vya kupambana na janga la moto, ikiwa ni maandalizi kupelekea kipindi cha kiangazi na kuimarisha ulinzi wa rasilimali za misitu.

Akizungumza wakati wa zoezi hilo, lililofanyika katika viwanja vilivyopo makao makuu ya shamba hilo, Msaidizi wa Mhifadhi Mkuu wa shamba hilo, ambaye pia ni Msimamizi wa kitengo cha uendelezaji rasilimali misitu na Nyuki, PCO. Said Singano amesema serikali imeendelea kuimarisha vikosi vya kuzuia na kupambana na moto kutokana na umuhimu wa kulinda misitu dhidi ya janga la moto. 

Sauti PCO. Singano 01

Amesema usaili huo umefanyika kwa kuzingatia vigezo na masharti yaliyowekwa, huku akibainisha nafasi zilizotangazwa kuwa ni 204 na waombaji ni zaidi ya 400, na lengo ikiwa ni kupata vijana wenye uwezo, watakaoshiriki kikamilifu katika shughuli hizo za kuzuia na kupambana na janga la moto ili kuhakikisha rasilimali hizo za misitu zinalindwa. 

Aidha, Ndgu. Singano amesema zoezi hilo litaendelea katika maeneo mengine ya wilaya hiyo, ikiwemo Tarafa ya Mgololo na Ihalimba, huku akiwaomba wale watakaokosa nafasi kutokukata tamaa bali waendelee kuomba fursa nyingine zitakapotangazwa.

Sauti PCO. Singano 02

Mmojawapo wa wasailiwa waliojitokeza katika mchakato huo wa kuomba kujiunga na vikosi vya kukabiliana na janga la moto katika shamba la miti Sao hill akifanyiwa usaili mbele ya wajumbe wa jopo la usaili ( Panelists members) uliofanyika katika makao makuu ya wakala huo, wilayani Mufindi. Picha na Kelvin Ayoub.

Kwa upande wao, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji wilayani humo, kupitia Sajenti. Guntram Mlenge amewataka wananchi kuacha tabia ya uchomaji moto ovyo, na kuwasihi wafuate taratibu mbalimbali wanazopaswa kuzifanya pindi wanapoandaa mashamba yao ili kuepusha janga hilo la moto katika misitu, huku akiahidi ushirikiano na TFS katika utoaji wa elimu kwa wananchi na uimarishaji wa vikosi hivyo vya kuzuia na kupambana na moto.

Sauti Sajenti. Mlenge

Nao baadhi ya wananchi waliohudhuria katika usaili huo, wamesema kazi ya kulinda misitu ni jukumu la kila mmoja, huku wakibainisha umuhimu wa shamba hilo la Sao hill katika maisha yao ikiwemo chanzo cha ajira na maendeleo ya uchumi kwa wakazi wengi wa wilaya hiyo na taifa kwa ujumla.

Sauti wasailiwa

Pichani ni waombaji waliojitokeza kuomba nafasi ya kujiunga na vikosi vya kuzuia na kupambana na janga la moto katika shamba la miti la Sao Hill wakifanyiwa usaili wa mazoezi ya kichura chura ili kupima utimamu wa mwili (Physical fitness). Picha na Kelvin Ayoub.

Zoezi hilo limeonesha mwitikio mkubwa kwa wananchi hao, na kudhihirisha dhamira yao ya ushiriki katika jitihada hizo za kuzuia na kupambana na janga la moto katika rasilimali za misitu hasa ikizingatiwa misitu ni maisha.