Mufindi FM
Mufindi FM
22 March 2026, 6:37 pm

Makundi yaliyo hatarini zaidi nchini yameendelea kukumbwa na changamoto kubwa katika upatikanaji wa huduma muhimu kufuatia athari za mabadiliko ya tabia nchi zinazozidi kushika kasi katika maeneo mbalimbali.
Na Marko Msafiri
Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) kupitia mradi wa “Ustahimilivu Wake, Dunia Yetu” (HROP) umetoa mafunzo maalum kwa waandishi wa habari wa mkoa wa Iringa, yakilenga kuimarisha uelewa kuhusu masuala ya kijinsia na mabadiliko ya tabia ya nchi.
Mafunzo hayo yamefanyika katika ukumbi wa Siasa ni Kilimo uliopo mkoani humo, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuhakikisha wanahabari wanaripoti kwa kina na kwa uwiano sawa kuhusu athari za mabadiliko ya tabia ya nchi.
Akizungumza baada ya mafunzo kutamatika Mwezeshaji, Deogratius Temba amesema kupitia waandishi wa habari kutasaidia kuharakisha kutimia kwa malengo madhubuti ya uanzishwaji wa mradi huo kwa jamii.
Aidha Ndg. Temba ameongeza kuwa, athari hizo za mabadiliko ya tabia nchi zimekuwa mwiba mkali kwa makundi hasa ya watoto, wanawake, vijana na wenye ulemavu, jambo linalohitaji nguvu ya wanahabari ili kusaidia kupunguza au kukomesha athari hasi zinagusa makundi hayo.

Nao washiriki wa mafunzo hayo wameahidi kuyatumia maarifa waliyoyapata kuboresha utendaji wao wa kazi hususani katika kuibua na kushughulikia changamoto zinazoikumba jamii na kwamba sauti na kalamu zao zitakuwa chachu ya mabadiliko chanya kwa makundi hayo yaliyo hatarini zaidi.

Mradi huo wa “Ustahimilivu wake, Dunia yetu” (HROP) unatekelezwa katika mikoa ya Iringa, Njombe na Mbeya.